Maoni

Wakazi wa Nyando wasusie kura hadi suluhu ya mafuriko ipatikane

Na CECIL ODONGO December 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAKAZI wa eneobunge la Nyando hawafai kupoteza muda wao na kuwachagua viongozi ambao wameshindwa kabisa kutatua janga la mafuriko ambalo limekuwa likisambaratisha maisha yao.

Huku maeneo mengine kama Budalang’i yaliyofahamika sana kwa mafuriko yakishuhudia maendeleo na hatua kubwa katika kupunguza janga hilo, eneo la Nyando watu wamebakia kivyao tena na mateso makubwa.

Ni majuma mawili tu yaliyopita ambapo mji wa Ahero ulisombwa na kuwasababishia wafanyabiashara hasara kubwa ilhali hakuna atakayewalipa fidia.

Nyando ni kitovu cha kilimo cha mpunga katika eneo la Nyanza ilhali Ahero ni mji ambao una shughuli nyingi kibiashara na una hifadhi ya mpunga.

Wakati ambapo mafuriko yanapotokea, wakulima hupata hasara nyingi baada ya mpunga wao kusombwa na maji ya mto Nyando ambao huvunja kingo.

Nyando ina wadi tano Awasi/Onjiko, Kobura, Kabonyo Kanyagwal na East Kano/Wawidhi na Ahero. Mbali na kilimo cha mpunga kushamiri sana, kuna kile cha miwa ambacho huathiriwa sana na mafuriko.

Wakazi wa maeneo haya hawajakuwa na amani kwa miaka mingi ambapo mafuriko yamekuwa yakisambaratisha maisha yao. Hadi leo, wengi bado hawana makao na wanaishi kambini.

Kuna wengi ambao hawana maboma kwa sababu walikokuwa wakiishi bado hakufikiwi kutokana na mafuriko.

Wengi hulazimika kuomba wenzao sehemu ya ardhi ya kuzika jamaa zao mauti yanapotokea huku mashirika ya kutoa misaada nayo yakionekana kupungua.

Katika wadi ya Kabonyo Kanyagwal, shule za msingi kama Kandaria, Kibarwa, Oseth, Odienya na Nyamrundi zilifunikwa na maji ya mafuriko.

Sehemu ambazo shule hizi zipo hazifikiwi na si salama kwa wanafunzi kusomea tena. Hii ndiyo maana Shule ya Msingi ya Ugwe na Nduru zimelazimika kutoa sehemu ya ardhi zao ili madarasa yajengwe kufaa wanafunzi kutoka shule za maeneo mengine yaliyosombwa na mafuriko.

Miundomsingi katika maeneo haya nayo ni duni huku barabara nyingi zikiwa hazina lami wala hazipitiki hasa wakati wa mafuriko.

Mbali na kutatizwa na mafuriko na njaa, wakazi pia wanapokea huduma duni za serikali huku viongozi wakionekana kutojali.

Kumekuwa na ahadi ya kujengwa kwa Bwawa la Koru-Soin ili kusaidia kukabili mafuriko lakini ahadi hiyo haijatimizwa licha ya kutumika kama chambo kila mara wakati wa kusaka kura.

Wakati mafuriko yalipotokea na kuzua uharibifu mkubwa mnamo Mei mwaka huu, msemaji wa serikali Isaac Mwaura alikuja na kusema kuwa serikali ingepatia kipaumbele ujenzi wa bwawa hilo linalogharimu Sh19.9 bilioni.

Kazi ya viongozi wa serikali na wale wa ODM imekuwa kuja na kuwapa raia maharagwe au mahindi gorogoro moja (kilo mbili) kisha kuhutubu na kuenda zao wakati mafuriko yanapotokea.

Hata sasa ambapo viongozi wa ODM wako serikalini, uongozi wote kutoka urais hadi udiwani hauonekani kufanya lolote baada ya mafuriko ya juzi.

Hakuna haja ya kupigia kura na kuwachagua viongozi ilhali raia wanateseka miaka nenda miaka rudi kutokana na tatizo lile lile.

Kupiga kura kwa wakazi wa Nuando ni kupoteza wakati na badala yake watafute suluhu nyingine au wakubali wamesahaulika na waendelee na mahangaiko yao.