Maoni

MAONI: Zogo baada ya Raila kushindwa uenyekiti AUC ni historia yetu

Na DOUGLAS MUTUA February 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NAANDIKA kuwakanya wafuasi wa kinara wa Muungano wa Azimio, Bw Raila Odinga, wanaowatukana wale wanaosherehekea kushindwa kwake katika jaribio la kuwa mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) hivi majuzi.

Nimesema kuwakanya – si kuwalaumu – kwa maana, labda kwa kuzidiwa na hasira, wamesahau jinsi siasa za Kenya zilivyo, wakawa wahanga wa mazoea yao wenyewe, tofauti ikawa kwamba leo wanalia wao.

Leo wanalia wao, jana walilia wengine, kesho watacheka wao, wengine watalia sana, kwa hivyo hamna haja ya kulaumiana wala kuoneana gere tunapojipata, kisiasa, kwenye misiba au karamu. Hivyo ndivyo maisha yalivyo.

Narejelea hali ilivyokuwa baada ya uchaguzi wa AUC mnamo 2017. Wakati huo, mwaniaji wa uenyekiti huo kutoka Kenya alikuwa Dkt Amina Mohamed, awali aliyewahi kuwa afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa, na waziri wa mambo ya nje pia.

Rais wa wakati huo alikuwa Uhuru Kenyatta, naibu wake Dkt William Ruto, Rais wetu wa sasa. Wawili hao walichukiwa hadi ya kuchukiwa na wananchi, kwa hivyo ushinde wa Dkt Amina ulishangiliwa kikweli ili kuwaudhi!

Sharti niseme kuwa Bw Odinga alikuwa mwaniaji mzuri, na mafedha yetu yalitumiwa kwa wingi kumfanyia kampeni kote barani Afrika, lakini bahati haikusimama. Si kosa lake, ni kosa la Kenya kama nchi, na ndiyo maana Mohammed Ali Yussuf wa Djibouti akamshinda

Mataifa mengi ya Afrika yanaamini Kenya ina kiherehere cha ama kuyatumia kujinufaisha, au kutumiwa na mataifa makuu na tajiri, hasa Amerika, kuyatawala kwa mbali. Iliyotuhini juzi ni migogoro ya maeneo ya kati, kusini na hata kaskazini mwa Afrika.

Inaaminika Muungano wa Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ulichukizwa nasi kutokana na vita vinavyoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kenya haiwezi kudai haifungamani na upande wowote katika vita hivyo; badala ya kuwapeleka askari wa kulinda amani na usalama Khartoum, iliwarusha kwa ndege hadi Haiti, na inaendelea kupokea hundi nono kutoka kwa Umoja wa Mataifa.

Ethiopia na Somalia pia hazikumchagua Bw Odinga. Bila shaka Kenya na Somalia zimekuwa na mzozo wa mpaka. Somalia ilipoingia mzozo wa aina hiyo na Ethiopia, ilikataa Kenya iwe mpatanishi.

Kenya ilishukiwa pia kuwaunga mkono waasi wa Tigray waliopigana na serikali ya Ethiopia miaka kadha iliyopita, na huenda ndiyo sababu Ethiopia ilimpa kura mwaniaji Yussuf wa Djibouti.

Kimsingi, Bw Odinga hakushindwa katika AUC kutokana na sababu zake binafsi bali kwa kuwa yeye ni Mkenya, na kwa sasa Kenya haijawa jirani mwema.

[email protected]