Habari

Marwa ashtakiwa kwa dai la kumtelekeza ‘mwanawe’

March 26th, 2019 1 min read

Na GERALD BWISA

MWANAMKE wa miaka 27 amefika katika mahakama moja ya Kitale akiitaka kumshinikiza Katibu wa Leba na Masuala ya Jamii Nelson Marwa kugharimia mahitaji ya mtoto wa mwaka mmoja anayedai ndiye baba yake halisi.

Anadai kwamba katibu huyo amekataa kugharimia mahitaji yake kama mzazi tangu kuzaliwa kwake.

Alisema kwamba wakati mtoto huyo alipozaliwa, Bw Marwa alimpa Sh50,000 kulipia ada ya hospitali.

Bi Moraa alisema kwamba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Bw Marwa ulioanza Januari 2017 uliopelekea mtoto huyo kuzaliwa mnamo Februari 2018.

Walipokutana na Bw Marwa, alikuwa akiishi Mombasa, alikohudumu kama Mshirikishi Mkuu wa eneo la Pwani.

“Nimeteseka sana kumlea mtoto huyu, ijapokuwa nimekuwa nikikumbana na changamoto nyingi. Kutokana na hali ngumu ya kiuchumi, huenda nikashindwa kabosa kumlea,” akasema kwenye taarifa iliyowasilishwa mahakamani.

Vile vile, alidai kwamba mshtakiwa amekataa kutoa kitambulisho chake ili mtoto huyo kupewa cheti cha kuzaliwa.

Hata hivyo, Bw Marwa amekanusha madai hayo, akikana kumfahamu mlalamishi kwa namna yoyote ile.

Kwenye taarifa yake kwa mahakama, Bw Marwa amesema kwamba hafahmu lolote kuhusu mtoto huyo.

Alisema kwamba alipokuwa akihudumu kama Mshirikishi Mkuu wa Ukanda wa Pwani, alikuwa akifanya mikutano na wananchi na maafisa wa serikali lakini hajawahi kuwa na mahusiano ya kimapenzi na yeyote.

“Sifahamu lolote kuhusu madai hayo. Hakuna wakati hata mmoja niliwahi kumsaidia mlalamishi kifedha kumlea mwanawe,” akasema.

Hakimu Mkuu Mkazi Cherono Kesse aliwapa wawili hao siku 14 kufika mbele ya mahakama, ili kuiwezesha kuagiza utafiti wa DNA katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH).

“Matokeo hayo yatawasilishwa mahakamani baada ya ukaguzi huo,” akasema.

Kesi hiyo itasikizwa tena mnamo Aprili 23.