Habari za Kitaifa

Mashahidi sasa kueleza ikiwa Mackenzie alihusika katika mauaji ya halaiki Shakahola

Na BRIAN OCHARO July 8th, 2024 2 min read

MBIVU na mbichi kuhusu mauaji ya Shakahola inatarajiwa kuanza kufafanuliwa mahakamani wiki hii wakati mashahidi wanatarajiwa kuanza kutoa ushahidi wao dhidi ya mshukiwa mkuu Paul Mackenzie na wenzake 93.

Mashahidi hao wamepangiwa kuanza kutoa ushahidi Jumatatu, Julai 8, 2024 kwenye kesi ambapo washukiwa wanakabiliwa na makosa kadhaa yanayohusiana na ugaidi.

Miongoni mwao ni mashahidi wanaolindwa ambao wanafahamu matukio ya msitu wa Shakahola ambayo yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 430 wanaoaminika kuwa waumini wa Kanisa la Good News International.

Kanisa hilo linahusishwa na Mackenzie na inaaminika kuwa lilitumika kama jukwaa la kupitishia itikadi kali mamia ya wafuasi wake ambao baadaye waliangamia wakiwa kwenye mfungo hatari wa kujitoa uhai.

Mfungo huo ulidaiwa kulenga kuwezesha wafuasi wote na Mackenzie kupaa mbinguni kukutana na “Yesu”.

Awali, mahakama ilisiambiwa kuwa Mackenzie alihubiri kanisani kwamba njia pekee ya kukutana na Yesu ni kwa kujiua kwa njaa.

Mashahidi hao wanatarajiwa kufichua kilichojiri katika msitu huo na jinsi wafuasi wa kanisa hilo walivyofundishwa itikadi kali kabla ya kukubali kufunga hadi kufa.

Zaidi ya hayo, mashahidi hao wanatarajiwa kufichua mafundisho waliyopokea, watu binafsi waliohusika na mafundisho haya, jinsi ujumbe ulivyowasilishwa, na maeneo mahususi na tarehe za shughuli hizi katika eneo la Furunzi huko Malindi kati ya 2020 na 2023.

Mackenzie, mkewe Rhoda Mumbua Maweu na wengine 93 wamekana makosa manne yanayohusiana na ugaidi.

Mackenzie almaarufu Mtumishi, Nabii au Papaa, Bi Maweu, Smart Mwakalama na mkewe Mary Kadzo Kahindi na wengine 28 walishtakiwa kwa makosa ya kujihusisha na uhalifu wa kupangwa na hivyo kuhatarisha maisha na kusababisha vifo vya wafuasi 429 wa kanisa hilo.

Mackenzie, Bi Maweu, Bw Kwakalama, mkewe na wenzake 28 pia wanashtakiwa kwa itikadi kali, ambapo serikali ilidai kuwa washukiwa hao waliendeleza mfumo wa imani uliokithiri kwa madhumuni ya kuwezesha vurugu za kiitikadi hadi kufa kwa kufunga hadi kufa kwa kuendeleza mabadiliko ya kidini.

Kundi lingine linalojumuisha Baron Chahenza na wenzake 63 wanashitakiwa kwa itikadi kali, ambapo serikali iliwatuhumu kwa kufuata mfumo wa imani uliokithiri kwa madhumuni ya kuwezesha vurugu za kiitikadi za kufunga hadi kufa.

Pia, walidaiwa kutumia mfumo wa itikadi kali kwa madhumuni ya kuendeleza mabadiliko ya kidini.

Mackenzie na Mwakalama wanakabiliwa na mashitaka tofauti kwa kosa la kuwezesha kufanyika kwa kitendo cha kigaidi. Serikali ilidai kuwa wawili hao kwa nia ya kufanya kitendo cha kigaidi, waliwezesha kufanyika kwa kitendo hicho kupitia  kuwasafirisha wafuasi wa kanisa lake kati ya msitu wa Shakahola na mji wa Malindi,  hivyo kuhatarisha maisha yao.

Mackenzie na mkewe pia wameshtakiwa kwa kosa la kumiliki video, vitabu na vipeperushi vya matumizi ya kuchochea kutendeka kwa kitendo cha kigaidi kwa kuhatarisha maisha ya waumini na wafuasi wa kanisa lake.

Serikali inadai kuwa washukiwa hao wawili walitenda makosa hayo katika eneo la Furunzi huko Malindi tarehe tofauti kati ya 2020 na 2023.