Habari za Kitaifa

Mashirika ya kijamii yaonya upinzani kukubali “mtego” wa Ruto


MASHIRIKA ya kijamii yamemtaka kiongozi wa upinzani Raila Odinga na wenzake kujihadhari na wito wa Rais William Ruto wa kushiriki mazungumzo ya kitaifa, yakisema Dkt Ruto haaminiki.

Baadhi ya mashirika hayo jana yalisema kuwa serikali ya Kenya Kwanza inasaka usaidizi kutoka kwa Odinga baada ya kung’amua kuwa imepoteza sifa machoni pa Wakenya kufuatia maandamano ya kuipinga.

Viongozi wa mashirika hayo wamemtaka Bw Odinga akatae kushiriki mazungumzo hayo wakati ambapo wazazi wa waathiriwa wa ukatili wa polisi wangali wanaombolewa wapendwa wao waliouawa huku wengi waliotekwa nyara wakiwa hawajapatikana.

Mkurugenzi Mkuu wa Muungano wa Kitaifa wa Mashirika ya Kijamii Suba Churchill alisema upinzani unapasa kupambana kuiondoa serikali hii mamlakani wala sio kuisaidia inaposhindwa kutekeleza ahadi zake “kupitia uundwaji wa serikali ya muungano”.

“Tunaushauri upinzani kuwa waangalifu zaidi na usikubali kuokoa serikali hii ambayo inaekelea kuporomoka kutokana na makosa yake. Upinzani utafakari kwa undani kuhusu wazo hilo kwani sisi kama mashirika ya kijamii hatudhani huu ni wakati mwafaka kwa Raila na wenzake kuisaidia serikali ya Ruto,

“Serikali hii  imewekosea Wakenya kwa kufeli kutimiza ahadi ilizotoa wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi wa 2022,” akasema Bw Churchill kwenye kikao na wanahabari.

Aidha, Bw Churchill na wenzake wanashuku nia ya Rais Ruto ya kuitisha mazungumzo hayo wakitaja hatua yake ya kuwateua tena mawaziri miongoni mwa wale aliowapiga kalamu Julai 11, 2024.

“Kwa kuharakisha kuwateua tena mawaziri sita aliowafuta kazi, Rais  amevuruga mazingira ya kuendeshea mazungumzo kwa njia nzuri. Hatua yake ilipasa kuandamanishwa na sababu zinazomfanya kushawishika kuwa sita hao ni bora kuliko wake wengine aliowapiga kalamu,” akaongeza Bw Churchill.

Miongoni mwa watu 11 ambao Rais Ruto aliwapendekeza kushikilia nyadhifa za uwaziri, sita ni wale waliohudumu katika baraza la zamani.

Wao ni; Aden Duale aliyependekezwa kuwa Waziri wa Ulinzi, Kithure Kindiki (Usalama wa Ndani), Soipan Tuya (Mazingira), Davis Chirchir (Barabara) (Alice Wahome) na (Rebecca Miano).

Bw Churchill na wenzake pia waliwaonya wabunge dhidi ya kuidhinisha majina ya sita hao wakisema hawafai kushikilia nyadhifa za uwaziri kwani maadili yao ni ya kutiliwa shaka.