Makala

Mauaji tata yaongezeka Nakuru hofu ikitanda


KAUNTI ya Nakuru inakumbwa na ongezeko mauaji ambayo hayajatatuliwa, na kuacha familia katika huzuni na jamii katika hofu na masikitiko.

Kuanzia kifo cha kusikitisha cha afisa wa polisi hadi mauaji ambayo hayajatatuliwa ya vijana wasio na hatia, visa kadhaa vya mauaji vinaonyesha kuna utepetevu ndani ya mfumo wa haki.

Mauaji ya Konstebo Harrison Onywoki Onwonga ni kimojawapo cha visa hivyo .

Mnamo Novemba 3, 2022, Konstebo Onwonga aliacha kazi yake katika kambi ya kikosi cha Recce eneo la Ruiru, Kiambu ili kuhudhuria mahafala ya mtoto wake wa miaka sita katika Kaunti ya Nakuru.

Baada ya sherehe hiyo, kijana huyo mwenye umri wa miaka 30 alipanga kukutana na kaka zake mjini ili kutazama mechi ya soka kabla ya kuelekea nyumbani.

Hata hivyo, jioni ilichukua mkondo wa kusikitisha walipokuwa Stimaline eneo la Mazembe, walipovamiwa na zaidi ya watu saba waliokuwa na silaha.

Onywoki alishambuliwa kikatili, akadungwa kisu, na kupigwa kwenye paji la uso. Licha ya kukimbizwa katika Hospitali ya Mama Kevin, mlinzi aliwakataza kuingia bila ripoti ya polisi, na hivyo kuwalazimisha kuripoti katika Kituo cha Polisi cha Kaptembwa.

Maafisa walipofahamu Onywoki alikuwa afisa wa polisi, alikimbizwa katika Hospitali ya Nakuru Level Five ambako alifariki saa kumi na moja kabla ya kupokea matibabu.

Visa vingine

Mnamo Februari 19, 2023, Elsie Waithera, msichana mwenye umri wa miaka mitatu, aliripotiwa kutoweka baada ya kuondoka nyumbani kupeleka maji kwenye kibanda cha nyanyake. Mwili wake ulipatikana katika shamba la mahindi saa mbili baadaye kufuatia msako mkali.

Kisa hicho hakijatatuliwa, na kuiacha familia katika dhiki kwa kukosa matokeo madhubuti ya uchunguzi.

Na mnamo Juni 4, 2023, mwili wa Beauty Njoki mwenye umri wa miaka 16, mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya St John katika Kaunti Ndogo ya Bahati, ulipatikana kwenye kichaka karibu na nyumba yao. Mjomba wa Njoki, Bw Joseph Waweru alisema alitoweka siku iliyotangulia, na mwili wake ukapatikana mchana siku iliyofuata.

Mamake Njoki Naomi Wanjiku anasema wapelelezi waliwaambia binti yake alivamiwa na kuuawa.

‘Tunachohitaji ni haki kwa binti yetu aliyekufa. Uchunguzi unapaswa kuharakishwa,” alisema.

Washukiwa wawili walikamatwa, lakini kucheleweshwa kwa uchunguzi wa DNA na masuala ya kiufundi kumezuia uchunguzi.

Daktari alipatikana amefariki

Mnamo Januari 2024, Dkt Labaan Kiptoo Langat, aliyekuwa na umri wa miaka 26 katika kitengo cha uzazi cha Margaret Kenyatta, alipatikana akiwa amefariki kwenye mtaro.

Dkt Langat alikuwa ameonekana akitoka kwenye sehemu ya burudani kabla ya mwili wake kugunduliwa.

Uchunguzi wa maiti ulionyesha kuwa alikufa kutokana na kunyongwa kwa mikono, akiwa na majeraha ya ziada kwenye shingo, kichwa, tumbo, viganja na midomo. Hakuna mshukiwa aliyekamatwa.

Na Julai 2023, Eileen Cherotich, mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Rift Valley alipatikana amefariki karibu na mzunguko wa Eveready kando ya barabara kuu ya Nakuru-Eldoret.

Cherotich alikuwa akirudi kutoka matembezi ya usiku na marafiki alipouawa.

Washukiwa wawili walizuiliwa kwa muda mfupi lakini baadaye waliachiliwa kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha kuwahusisha na uhalifu huo.

Mnamo Jumatatu Septemba 17, 2024, Afisa Mkuu wa DCI wa Nakuru Magharibi Charles Kamau alithibitisha kuwa uchunguzi unaendelea huku mamlaka ikimsaka mshukiwa mkuu ambaye bado yuko huru.