Habari Mseto

MCK yasitisha vibali vya wanahabari watatu waliopigana

January 26th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

BARAZA la Wanahabari Nchini limesitisha vibali vya wanahabari watatu waliofanya vita katika mkutano wa umma Januari 20, 2024 Kaunti ya Siaya.

Afisa Mkuu mtendaji wa Baraza hilo, David Omwoyo aliongoza mkutano wa kubaini kilichojiri na Baraza hilo kuamuru vibali vya Josiah Odanga (Radio Africa -The Star), George Amolo (Royal Media Services – Ramogi) na Mary Goretty Juma (Mediamax Network) kusitishwa mara moja.

“Kulingana na jinsi walivyokiri kwa kujihusisha na tabia zisizoambatana na maadili ya taaluma kama vile kupigania hongo, Baraza limesitisha kuidhinishwa kwao hadi ilani nyingine itakapotolewa,” Bw Omwoyo aliwafahamisha watatu hao.

Pia, Baraza hilo limewasiliana na wahariri wa vyumba vya habari wanakofanya kazi. Wahariri wasimamizi walifahamishwa jinsi watatu hao walikiuka maadili ya uandishi wa habari nchini.

“Tunaamini tumewapa wanahabari hao haki kwa kuwasikiliza na kwamba uamuzi wa baraza hili ni kuweza kurejesha nidhamu katika taaluma hii,” alisema Bw Omwoyo.

Uamuzi huu unatokana na jukumu la MCK, lililotolewa na Sheria ya Baraza la Vyombo vya Habari, 2013, kukuza na kulinda uhuru wa vyombo vya habari pamoja na kuimarisha viwango vya maadili na kitaaluma miongoni mwa wanahabari na kampuni za kutoa habari.