Habari Mseto

Mfanyabiashara kizimbani kwa ulaghai wa shamba la Sh1.6 bilioni

Na RICHARD MUNGUTI August 29th, 2024 1 min read

MFANYABIASHARA alishtakiwa mnamo Jumanne, Agosti 27, 2024 kwa kula njama za kulaghai kampuni ya uwekezaji katika nyanja ya viwanda shamba la hekta 21 ya thamani ya Sh1.6 bilioni.

Francis Muhuhu Ndinguri alishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Martha Nanzushi.

Ndinguri alikana mashtaka matatu dhidi yake aliposomewa na hakimu.

Bi Nanzushi alimweleza mshtakiwa kwamba Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Renson Ingonga amemfungulia mashtaka kwamba akishirikiana na watu wengine, kati ya Januari 4 na Septemba 15, 2023 walikula njama za kulaghai Kampuni ya Langton Investments Limited (LIL).

Bi Nanzushi alimfahamisha mshtakiwa shamba hilo ni la hekta 21.85 la thamani ya Sh1, 619, 700,000.

Shamba hilo, Ndinguri alielezwa liko katika Northern Bypass eneo la Embakasi Kaunti ya Nairobi.

Shtaka la pili dhidi ya Ndinguri lilisema kwamba  mnamo Feburuari 23, 2023, mahala pasipojulikana humu nchini alighushi cheti cha usajili cha kampuni ya LIL katika afisi za Mwanasheria Mkuu.

Mfanyabiashra Francis Muhuhu Ndinguri akiwa katika Mahakama ya Milimani mnamo Agosti 27, 2024 kwa kesi ya utapeli wa shamba lenye thamani ya Sh1.6 bilioni. WILFRED NYANGARESI|NATION

Shtaka la tatu dhidi ya Ndingur, lilisema kati ya Januari 4 na Septemba 15 2024 katika Wizara ya Ardhi alijipatia cheti cha cha muda cha umiliki wa ardhi hiyo akijifanya alikuwa mkurugenzi wa Langton Investment Limited.

Mahakama ilielezwa na kiongozi wa mashtaka, Bi Ann Munyua kwamba Ndinguri aliipa Wizara ya Ardhi cheti Nambari 78508 akidai alikuwa Mkurugenzi wa LIL.

Shtaka lilisema alikuwa na lengo la kujipatia cheti cha umiliki wa shamba hilo la hekta 21.85.

Mshtakiwa aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana, akisema atafika kortini wakati wa kusikizwa kwa kesi inayomkabili.

Bi Munyua hakupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Hakimu alimwachilia Ndinguri kwa dhamana ya Sh1 milioni, pesa tasilimu.

Kesi imeorodheshwa kusikizwa Oktoba 4, 2024

[email protected]