ADUNGO: Tusidanganyane, ligi kuu msimu huu ni ya farasi 2; Liverpool na Manchester City
Na CHRIS ADUNGO
MANCHESTER City walifanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu uliopita.
Masogora hawa wa kocha Pep Guardiola walijizolea jumla ya alama 98 na kuwapiku Liverpool walioambulia nafasi ya pili kwa alama 97 kutokana na mechi 38.
Ilivyo, dalili zote zimeashiria kwamba farasi wawili katika kampeni za EPL msimu huu bado watakuwa Man-City na Liverpool ambao kwa sasa wanaongoza kilele cha jedwali baada ya kusajili ushindi katika mechi zao saba za ufunguzi wa muhula huu.
Je, kuna kikosi chochote kilicho na uwezo wa kuwapiga Liverpool breki msimu huu kadri wanavyowania ubingwa wa taji la EPL? Kufikia sasa, Liverpool ndio wa pekee ambao wameashiria kwamba wana uwezo kuwakaba koo miamba wote katika soka ya Uingereza. Wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 21 wakijivunia jumla ya mabao 18. Nyavu zao zimetikiswa mara tano pekee na pengo la pointi tano linatamalaki kati yao na Man-City ambao wangali katika nafasi ya pili.
Je, hali itakuwaje kwa Chelsea ambao chini ya kocha mpya Frank Lampard wameanza kuzoea maisha bila ya huduma za Eden Hazard na David Luiz waliohamia Real Madrid na Arsenal mtawalia? Je, Tottenham Hotspur waliopoteza jumla ya mechi 13 msimu jana, wana uwezo wa kuendea ubingwa wa EPL mara hii? Arsenal watafanikiwa kurejea kushiriki kampeni za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) baada ya kukaa nje kwa miaka mitatu?
Na je, Man-United wana uwezo wa kuwa wagombezi halisi wa taji la EPL baada ya kushindwa kabisa kuukaribia ufalme huo katika kipindi cha miaka sita iliyopita?
Kwa mara nyingine, nahisi kwamba kampeni za EPL muhula huu zitashuhudia ushindani mkali kati ya klabu mbili za kwanza na nne nyinginezo ambazo zitakuwa zikiwania nafasi mbili za ziada za kufuzu kwa kipute cha UEFA msimu ujao.
Kubwa zaidi ambalo wakufunzi Pep Guardiola na Jurgen Klopp walifanikiwa kwalo msimu jana, ni kuwapa mashabiki wa soka ya EPL burudani tosha na kitu kipya cha kufuatilia zaidi katika msimu huu mpya wa kipute hicho.
Katika msimu wake wa tatu uwanjani Etihad, Guardiola ambaye ni mzaliwa wa Uhispania alifaulu kuwachochea masogora wake wa Man- City kupiga soka safi zaidi yenye pasi za uhakika kama walivyokuwa wakicheza Barcelona wakati mkufunzi huyu alipokuwa akidhibiti mikoba ya miamba hao wa soka ya Uhispania.
Chini ya Guardiola, Man-City kwa sasa wamedhihirisha kwamba wana uwezo wa kutandaza soka ya kuvutia katika michuano yote ya haiba kubwa ndani ya Uingereza na kwenye mapambano ya bara UEFA.
Tottenham, Chelsea na Arsenal waliokuwa wawe wapinzani wa wakuu wa Man-City na Liverpool, wamekuwa wakisuasua.
Ishara za ukubwa
Licha ya Tottenham, Man-United na Arsenal kuonyesha ishara za ukubwa wa kiu yao katika jitihada za kutawazwa mabingwa wa EPL msimu huu, mtandao wa Mirror Football nchini Uingereza bado umewapa Liverpool na Man-City nafasi kubwa ya kupiku wapinzani wao wakuu kwa mara ya tatu mtawalia na matokeo ya hadi kufikia sasa yanathibitisha hivyo.
Chini ya Guardiola, Man-City wanapigiwa upatu wa kumaliza kivumbi cha EPL msimu huu katika nafasi ya pili nyuma ya Liverpool huku Chelsea wakiwekwa katika nafasi ya tatu mbele ya Arsenal na Tottenham.
Man-United ambao wanatarajiwa kuambulia nafasi ya sita, huenda wakamtema mkufunzi Ole Gunnar Solskjaer na nafasi yake kutwaliwa na Mauricio Pochettino ambaye kuondoka kwake Tottenham kutampisha kocha wa timu ya taiga ya Uingereza, Gareth Southgate.