• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 3:55 PM
Aibu ya Marwa kujinyima mamilioni kwa kukubali hongo ya Sh60,000

Aibu ya Marwa kujinyima mamilioni kwa kukubali hongo ya Sh60,000

 

Na GEOFFREY ANENE

REFA Aden Range Marwa amepoteza posho ya Sh2,521,250 angepata kwenye Kombe la Dunia nchini Urusi na nyongeza ya Sh 201,691 kutoka kila mechi angesimamia kati ya Juni 14 na Julai 15.

Hii ni baada ya mwalimu huyu wa somo la hisabati na kemia katika Shule ya Upili ya Kotombo kutoka Kaunti ya Migori, kunaswa kwenye kamera akipokea hongo ya Sh60,000 kupanga matokeo ya mechi moja ya kimataifa.

Kufuatia ufichuzi wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC), Aden Range Marwa, 41, ametemwa kutoka orodha ya maafisa wa kusimamia mechi.

Marwa alikuwa katika orodha ya marefa 63 wasaidizi walioteuliwa kunyanyua kibendera katika kindumbwendumbwe hiki.

Ufichuzi wa BBC ulifanywa na ripota mmoja kutoka Ghana Anas Aremeyaw Anas na unafichua Marwa pamoja na makumi ya marefa wengine wakidaiwa kupokea fedha hizo.

Picha hizo za video zinaonyesha Marwa akipokea fedha katika sehemu inayoonekana kuwa katika chumba chake hotelini.

Mdai wake anasema picha hizo zilinaswa wakati wa Soka ya Afrika ya wachezaji wanaosakata katika ligi zao (CHAN) nchini Morocco mwaka huu.

Cha kushangaza ni kwamba Mkenya huyo mwenye umri wa miaka 41 anasikika akikubali fedha hizo kama zawadi na hata kuwa tayari kuendeleza urafiki huo.

“Unajua, asante kwa zawadi, lakini cha muhimu sana ni kuendeleza urafiki huu,” anasema Marwa.

Refa huyu, ambaye aliibuka refa bora msaidizi nchini Kenya mwaka 2017, hakupatikana kuzungumzia ufichuzi huo, lakini Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Nick Mwendwa ameahidi kuchunguza kesi hiyo.

“Tumepokea madai hayo kupitia kwa vyombo vya habari,” alisema Mwendwa.

“Kwa hivyo, tunataka kesi hii ifuate mkondo wake. Ni muhimu kufahamu kwamba kama Shirikisho, bado hatujapokea malalamishi kuhusu afisa huyu, iwe katika maandishi, kupitia kinywa ama ishara.”

“Hata hivyo, msimamo wetu kama FKF ni kwamba haturuhusu kabisa visa vya ufisadi, lakini pia tunaamini kabisa katika haki na usawa kwa wote. Hiyo ndiyo sababu tutakuwa tukikutana naye katika siku zijazo kusikia maoni yake kabla ya kutangaza rasmi msimamo wetu kuhusu kesi hii hata tunaposubiri uchunguzi wowote kutoka kwa Fifa.”

Marwa alikuwa katika mwaka wake wa saba kama refa wa Fifa.

Alikuwa katika orodha ya maafisa wa kusimamia mechi katika makala yaliyopita ya Kombe la Dunia nchini Brazil mwaka 2014, lakini hakupewa mechi ya kusimamia.

Alikuwa refa msaidizi katika mashindano ya dunia ya Klabu Bingwa ya mwaka 2016 nchini Japan.

Pia alikuwa katika orodha ya marefa kutoka Afrika waliosimamia Kombe la Mashirikisho nchini Urusi mwaka 2017, akahudumu katika mashindano ya Afrika (AFCON) mwaka 2012, 2013 na 2015 pamoja na CHAN, Kombe la Dunia la Under-17, Kombe la Afrika la Under-23 na mashindano ya dunia ya Klabu Bingwa.

You can share this post!

Kenya, Uganda na TZ zashuka viwango vya FIFA

KOMBE LA DUNIA: Eriksen aondoka kambini kusherehekea mtoto...

adminleo