Arsenal matumaini yote sasa ni kwa Kombe la FA
Na MASHIRIKA
LONDON, Uingereza
MKUFUNZI wa Arsenal, Mikel Arteta amewataka vijana wake kuweka kando maruerue ya kubanduliwa nje ya kipute cha Uropa, na kuweka hai matumaini ya kutwaa ubingwa wa Kombe la FA muhula huu.
Arsenal watakuwa leo Jumatatu wageni wa Portsmouth katika mechi ya raundi ya tano ya FA, itakayosakatiwa uwanjani Fratton Park.
Kombe hilo ndilo limebakia kuwa fursa ya pekee kwa Arsenal kuingia katika michuano ya Ulaya. Hii ni kwa sababu mshindi wa FA huingia moja kwa moja katika kipute cha Uropa katika awamu ya makundi.
Arsenal kwa sasa wana alama 37 katika Ligi Kuu (EPL) na matumaini yao ya kufuzu kwa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao ni finyu sana, ikizingatiwa kuna pengo la pointi nane kati yao na Chelsea, wanaofunga mduara wa nne-bora wa kujitosa katika kipute hicho cha klabu bingwa.
Kikosi cha Arteta kinapigiwa upatu kuibuka na ushindi hii leo dhidi ya Portsmouth, baada ya gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) lililokuwa liwakutanishe na Manchester City wikendi iliyopita, kuahirishwa.
Kiini cha kusongezwa mbele kwa kivumbi hicho cha ligi ni fainali ya Carabao Cup, ambayo Man-City ilicheza jana na Aston Villa katika uwanja wa Wembley, Uingereza.
Arsenal watajitosa uwanjani dhidi ya Portsmouth siku nne tu baada ya kuondolewa na Olympiacos kwenye kipute cha Uropa, kwa kanuni ya bao la ugenini licha ya kutoka sare ya 2-2 mwisho wa michuano hiyo ya mikondo miwili.
Akihojiwa baada ya mazoezi Jumamosi, Arteta alidokeza uwezekano wa kuwaacha nje masogora Mesut Ozil na Alezandre Lacazette katika kikosi atakachokitegemea leo dhidi ya Portsmouth.
Hatua hiyo inamaanisha lazima atawajibisha Nicolas Pepe na Eddie Nketiah katika safu ya mbele, itakayoongozwa na nahodha Pierre-Emerick Aubameyang ambaye kwa sasa anawaniwa pakubwa na klabu za Barcelona na Inter Milan.
Aubameyang anashikilia uongozi wa orodha ya wafungaji bora wa ligi kwa mabao, sawa na Jamie Vardy wa Leicester City.
Kwa mujibu wa gazeti la Express Sport nchini Uingereza, Aubameyang atakuwa radhi zaidi kuondoka uwanjani Emirates mwisho wa msimu iwapo Arsenal itakosa kufuzu UEFA muhula ujao.
Kwa kutofuzu UEFA msimu uliopita, Arsenal walikosa Sh3.8 bilioni. Tayari wamekosa pia zaidi ya Sh1.2 bilioni ambazo wangelipokezwa iwapo wangelitinga hatua ya 16-bora ya Uropa msimu huu.