Michezo

Arsenal waliolipua Burnley Jumamosi wakosa risasi katika Uefa

February 22nd, 2024 2 min read

NA MASHIRIKA

PORTO, URENO:

KAMBI ya Arsenal imejaa masikitiko baada ya kupigwa bao moja chungu na FC Porto dakika ya mwisho katika mechi ya duru ya kwanza ya raundi ya 16-bora kwenye soka ya Klabu Bingwa Ulaya nchini Ureno, Jumatano.

Vijana wa kocha Mikel Arteta walikuwa wameshinda michuano mitano mfululizo kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa jumla ya mabao 21-2.

Wanabunduki hao walijibwaga uwanjani Dragao wakiwa na matumaini makubwa, lakini wakalazimika kukunja mkia baada ya kukosa kulenga hata shuti moja langoni, mara yao ya kwanza kufanya hivyo kwenye soka ya UEFA tangu Machi 2011 dhidi ya Barcelona.

Arsenal sasa ni klabu ya tano kupoteza mara tano mfululizo ugenini kwenye awamu ya muondoano ya Klabu Bingwa Ulaya baada ya Real Madrid (Februari 2010), Celtic (Machi 2013) Leverkusen (Machi 2014) na Roma (Februari 2018).

Soma pia Man U wakanyaga shingo Aston Villa, huku Arsenal wakilipua West Ham bila huruma

Vijana wa Arteta pia hawajashinda Porto nchini Ureno mara nne mfululizo baada ya kutoka 0-0 Desemba 2006 kabla ya kuangamizwa 2-0 (Desemba 2008), 2-1 (Februari 2010) na sasa 1-0 (Februari 2024).

Hata hivyo, Arsenal wana rekodi nzuri dhidi ya Porto jijini London, Uingereza. Wameshinda mechi tatu mfululizo kwa jumla ya mabao 11-0.

Hata hivyo, kichapo kinawaweka Wanabunduki hao katika hatari ya kubanduliwa wasipotawala mechi ya marudiano hapo Machi 12.

Hapo Jumatano, Mbrazil Galeno alimwaga kipa David Raya kupitia kombora kali nje ya kisanduku katika dakika ya mwisho ya majeruhi baada ya Arsenal kupoteza mpira kutokana na pasi mbovu kutoka kwa Gabriel Martinelli katika ya uwanja.

“Inasikitisha tulivyoachilia mechi hii dakika ya mwisho. Kama huwezi kushinda haifai upoteze,” alichemka Arteta akisema vijana wake walitawala mechi, lakini wakakosa lengo la kutatiza safu ya ulinzi ya Porto.

Soma pia Jinsi Arsenal waliitoa Liverpool pumzi

“Tutajifunza kutokana na mchuano huu. Tuko mapumzikoni. Ukitaka kuwa katika robo-fainali, lazima upige mpinzani wako. Tulikosa makali leo,” akasema Mhispania huyo.

Mashabiki wamlimkosoa Raya vikali kwa kutomakinika michumani wakati wa kufungwa bao hilo kwani alikuwa ametoka sana kwenye laini ya goli.

“Bila shaka, matokeo haya yanasikitisha, lakini tuko mapumzikoni. Bado kuna mechi ya marudiano nyumbani na hatuna budi kutwaa ushindi,” akasema Raya aliyejaa matumaini kuwa Arsenal wana uwezo wa kuvuna ushindi ugani Emirates, London.

Katika mechi nyingine Jumatano, mwanasoka bora wa Afrika mwaka wa 2023 Victor Osimhen alinasua Napoli iliyohepa hatari ya kuchapwa nyumbani kwa kuzoa sare ya 1-1 na Barcelona.

Robert Lewandowski aliweka Barca kifua mbele dakika ya 60 kabla ya Osimhen kusawazisha dakika ya 75.