Arsenal yajipiga kifua, Arteta akionya Liverpool
LONDON, Uingereza
MIKEL Arteta ameonya Liverpool kuwa Arsenal wamerejea kwenye vita vya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kuonyesha ujasiri wakilemea majirani Tottenham Hotspur 2-1 mbele ya mashabiki 60, 287 ugani Emirates, Jumatano, Januari 15, 2025.
Wanabunduki wa Arsenal walihitaji ushindi huo vibaya sana ili kupunguza mwanya kati yao na viongozi Liverpool na walifanya hivyo baada ya kutoka nyuma bao moja.
Son Heung-min alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 25 kabla ya Dominic Solanke kusawazishia Arsenal 1-1 kwa kujifunga kutokana na kona baada ya kugusa mpira wa kichwa kutoka kwa Gabriel Magalhaes dakika ya 40.
Leandro Trossard kisha alipachika bao la ushindi kutokana na asisti ya nahodha Martin Odegaard dakika ya 44 baada ya kumwaga kipa Antonin Kinsky.
Ushindi wa pili wa Arsenal dhidi ya Spurs ligini msimu huu na watatu mfululizo tangu msimu 2023-2024 umefanya wanabunduki warukie nafasi ya pili kutoka nambari tatu.
Wana alama 43, nne nyuma ya vijana wa kocha Arne Slot walio na mechi moja mkononi.
“Bado tupo katika vita vya kuwania taji. Kuna alama nyingi mezani za kupigania, lakini hakuna mechi rahisi,” akasema Arteta.
“Unapopata fursa ya kukata mwanya huna budi kuitumia vyema. Tunafurahia matokeo ya leo na kuzamia maandalizi ya mchuano ujao. Nimefurahishwa na kazi vijana wamefanya. Nadhani walikuwa juu,” akaongeza Arteta.
Alikiri kuwa mchuano huo ulikuwa mtihani mkubwa uliokuja baada ya kutoka 1-1 na Brighton ligini na kupoteza dhidi ya Newcastle 2-0 (Kombe la Carabao) na 5-3 mikononi mwa Manchester United (Kombe la FA).
“Ulikuwa mtihani mkubwa baada ya kuambulia pakavu katika mashindano mawili tofauti. Ulikuwa mtihani wa kiakili na ujasiri. Tulijituma kutoka dakika ya kwanza na kucheza tukiwa na lengo la kuwatwanga…Ilikuwa mechi muhimu na tunafurahia kuwapa mashabiki zawadi ya kufurahia,” akasema Arteta.
Kocha wa Spurs, Ange Postecoglou, ambaye alisisitiza kuwa Arsenal hawakustahili kupata iliyozalisha bao la kusawazisha, aliponda vijana wake akisema hawakuonyesha uhai, hasa katika kipindi cha kwanza.
“Tuliwapa Arsenal nafasi ya kudhibiti mechi. Kipindi cha pili kilikuwa kizuri kidogo, lakini hatukukaribia viwango vya juu,” akasema Postecoglou.
Ripoti zinasema kuwa Postecoglou ananing’nia pabaya kufutwa kazi.
Spurs sasa wamepoteza michuano 11 ligini, idadi kubwa baada ya mechi 21 katika msimu mmoja tangu msimu 2008-2009.
Katika mechi nyingine Jumatano, Newcastle walizoa ushindi wa sita mfululizo baada ya kulipua wageni Wolves 3-0 kupitia mabao ya Alexander Isak (mawili) na Anthony Gordon, nao Jean-Philippe Mateta na Marc Guehi wakafungia Crystal Palace katika ushindi wa 2-0 dhidi ya wenyeji Leicester.
Naye kocha David Moyes alianza maisha vibaya kambini mwa Everton baada ya vijana wake kuzamishwa 1-0 na Ollie Watkins wa Aston Villa ugani Goodison Park.