Arsenal yapepeta Bournemouth mechi za ‘pre-season’ zikianza rasmi
ARSENAL FC walianza mechi za kujiandaa kwa msimu 2024-2025 kwa kulemea Bournemouth kwa njia ya penalti 5-4, Alhamisi.
Timu hizo zilitoka sare ya 1-1 katika muda wa dakika 90 baada ya winga Fabio Vieira kujaza kimiani krosi ya Reiss Nelson kwa ustadi katika dakika ya 18 naye Antoine Semenyo akasawazishia Bournemouth dakika ya 73 ugani Dignity Health Sports Park.
Kipa Karl Hein kutoka Estonia alikuwa nyota wa Arsenal baada ya kupangua penalti mbili na pia kuridhisha wakati wa mechi.
Alizima mshambulizi matata Dominic Solanke na alifungwa na Semenyo baada ya kombora la winga huyo kuguswa na mchezaji wa Arsenal.
Waliofungia Arsenal katika upigaji wa penalti ni Martin Odegaard, Oleksandr Zinchenko, Jorginho, Gabriel Jesus na Jakub Kiwior.
Bournemouth walipachika wavuni penalti zao kupitia kwa Semenyo, Dango Ouattara, Adam Smith na Daniel Jebbison.
Hein alipangua penalti ya Philip Billing na Ryan Christie naye Leandro Trossard aliuza penalti yake kwa upande wa wanabunduki.
Mechi ijayo ya kirafiki ya Arsenal ni dhidi ya Manchester United ugani SoFi, Los Angeles hapo Julai 27.
Matokeo ya kirafiki
Julai 24: Manchester City 3-4 Celtic, Bordeaux 2-3 Southampton, Kashima Antlers 1-5 Brighton, Fulham 4-0 QPR
Julai 25: Arsenal 5-4 Bournemouth, Chelsea 2-2 Wrexham.