Michezo

Arsenal yapewa asilimia kubwa kushinda Klabu Bingwa Ulaya kuliko Real Madrid

Na GEOFFREY ANENE April 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ARSENAL wana asilimia kubwa ya kushinda Klabu Bingwa Ulaya 2024-2025 kuliko mabingwa watetezi Real Madrid.

Ubashiri wa hivi punde wa kompyuta maalum ya Opta umejumuisha wanabunduki miongoni mwa timu zilizo na asilimia zaidi ya 10 ya kushinda mashindano hayo ya haiba.

Katika ubashiri wake, Opta imewapa viongozi wa Ligi Kuu ya Uhispania Barcelona uwezo mkubwa wa kutwaa ubingwa wakiwa na asilimia 23.1.

Mabingwa wa Ligi Kuu ya Ufaransa, Paris Saint-Germain wanafuata Barca kwa asilimia 19.3, Arsenal wana asilimia 15.6, Inter Milan 13.8, nao washikilizi wa rekodi ya mataji mengi ya kipute hiki Real Madrid (wameshinda mara 15) wamepewa asilimia 12.2.

Bayern Munich wanafunga orodha ya timu zilizo na asilimia juu ya 10 ya kunyakua taji la ligi hiyo ya klabu 36 itakayoingia robo-fainali hapo Aprili 8.

Katika orodha ya timu zilizofuzu kushiriki robo-fainali ni Aston Villa na Borussia Dortmund pekee wamepewa asilimia ndogo ya kutawala dimba hilo.

Villa wana asilimia 3.7 nao Dortmund 1.5.

Arsenal watavaana na Madrid, Bayern wapepetane na Inter, Barcelona walimane na Dortmund nao PSG watakabana koo na Villa katika robo-fainali katika mechi za mkondo wa kwanza za robo-fainali hapo Aprili 8-9. Marudiano ni Aprili 15-16.

Ni mechi za kufa-kupona kumaanisha uwezo wa timu kutwaa taji utafifia ikipoteza katika mkondo wa kwanza. Nusu-fainali ni Aprili 29-30 na Mei 6-7 nayo fainali itasakatwa Mei 31.

Arsenal walibandua Madrid katika raundi ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya msimu 2005-2006.

Wanabunduki walichapa Madrid 1-0 ugani Santiago Bernabeu (Februari 21, 2006) kabla ya kulazimisha 0-0 mjini London (Machi 8, 2006) katika raundi ya 16-bora.

Msimu huo unasalia mzuri kabisa wa Arsenal katika Klabu Bingwa Ulaya baada ya kufika fainali na kupoteza 2-1 dhidi ya Barca.

Arsenal walipasha misuli moto kwa mchuano huu kwa kutoka 1-1 dhidi ya Everton ligini nao Madrid waliduwazwa 2-1 na Valencia wanaopigania kukwepa kushusha daraja kutoka LaLiga.

Kivumbi kitakuwa kati ya mabingwa wa zamani Bayern na Inter ambao wanaongoza Ligi Kuu ya Ujerumani na Italia, mtawalia.

Hata hivyo, Bayern ambao wana mkali Harry Kane, wamechabanga Inter mara tatu mfululizo katika dimba hilo kwa jumla ya mabao 5-0.

Barca wanaojivunia kuwa na mfumaji matata Robert Lewandowski, walipiga Dortmund 3-2 katika makundi Desemba 2024.

Kocha wa Barca, Hansi Flick ameshinda Dortmund mara yote sita amekutana nayo.

Mechi ya PSG na Villa ni vita vya timu zilizo katili zaidi wakati huu. PSG, ambao wana mshambulizi matata Ousmane Dembele, wamezoa ushindi mara sita mfululizo katika mashindano yote nao Villa wanafukuzia ushindi wa 10 mfululizo katika mashindano yote.