Arsenal yapoteza asilimia 7.9 ya kushinda EPL
ARSENAL imepoteza asilimia kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza baada ya matokeo ya mechi za Novemba 8-9 kuchambuliwa na kompyuta ya Opta.
Vijana wa kocha Mikel Arteta walitolewa kijasho wakitoka 2-2 ugani Stadium of Light dhidi ya wenyeji Sunderland wanaorejea kwenye ligi hiyo ya klabu 20 tangu msimu 2026-2017.
Wanabunduki hao bado wamepewa aslimia kubwa ya kumaliza msimu 2025-2026 juu ya jedwali. Wamepewa na Opta uwezo wa asilimia 63.60 wa kuibuka mabingwa baada ya kila timu kusakata michuano 11. Wanaongoza jedwali kwa alama 26.
Manchester City wameimarisha asilimia yao ya kunyakua taji kutoka 13.5 hadi 22.94 baada ya kulipua mabingwa watetezi Liverpool 3-0 ugani Etihad. Vijana wa kocha Pep Guardiola wanakamata nafasi ya pili kwa alama 22.
Liverpool wamepewa asilimia 7.01 ya kuhifadhi taji. Vijana wa kocha Arne Slot walikuwa na asilimia 9.7 baada ya kutwanga Aston Villa 2-0 katika wiki ya 10. Kwenye jedwali, Reds wanapatikana katika nafasi ya nane wakiwa na alama 18.
Chelsea wameimarisha asilimia yao ya kushinda ligi kutoka 1.8 hadi 2.75 baada ya kulambisha sakafu Wolves 3-0 ugani Stamford Bridge. Blues wako nambari tatu kwenye jedwali kwa alama 20.
Katika ubashiri wa Opta, Bournemouth wamepoteza uwezo wao kutoka asilimia 0.8 hadi 0.37 baada ya kuumizwa 4-0 na Aston Villa, Crystal Palace wameimarika kutoka asilimia 0.8 hadi 0.85 licha ya kutoka sare tasa dhidi ya Brighton nao Villa wameongeza asilimia yao kutoka 0.7 hadi 1.30.
Uwezo wa Tottenham wa kutwaa taji umeshuka kutoka asilimia 0.40 hadi 0.22 baada ya kutoka 2-2 dhidi ya Manchester United ambao uwezo wao umeongezeka kutoka asilimia 0.3 hadi 0.41.
Brighton, Newcastle na Brentford ni timu nyingine zilizo na uwezo wa kunyakua taji katika ubashiri huo wa Opta. Brighton wameimarika kutoka asilimia 0.3 hadi 0.32 nao Newcastle wameshuka kutoka 0.2 hadi 0.11 baada ya kupokea kipigo cha 3-1 kutoka kwa wenyeji Brentford ugani Gtech.
Brentford, ambao hawakuwa wamepewa uwezo wa kutawala ligi hiyo, sasa wana asilimia 0.12 ya kufanya hivyo.
Kwenye jedwali, Sunderland wanakamata nafasi ya nne kwa alama 19, wakifuatiwa na Tottenham, Villa, mashetani wekundu wa United, Liverpool na Bouremouth (wote alama 18), Palace (17), Brighton na Brentford (16), Everton (15) na Newcastle (12).
Licha ya Sunderland kuwa nambari nne, washiriki hao wapya kwa jina la utani Black Cats wamepewa asilimia 0.0 ya kushinda ligi. Wako kapu moja na Everton (wana pointi 15), Fulham (11), Leeds (11), Burnley (10), West Ham (10), Nottingham Forest (tisa) na Wolves (mbili).