Barcelona wapunguza bei ya Umtiti kwa zaidi ya asilimia 50 kuwavutia Arsenal
Na CHRIS ADUNGO
BARCELONA wamepunguza bei ya difenda wao Samuel Umtiti, 26, kwa asilimia kubwa kutoka Sh6.3 bilioni hadi Sh3.7 bilioni ili kumwezesha kuondoka ugani Nou Camp na kujiunga na Arsenal.
Hata hivyo, Arsenal watalazimika kuwapiga kumbo watani wao wakuu katika soka ya Uingereza, Manchester United ili kujinasia huduma za Umtiti ambaye ni mzawa wa Ufaransa.
Barcelona ambao ni miamba wa soka ya Uhispania ni miongoni mwa klabu ambazo zimeathiriwa pakubwa zaidi kifedha na janga la corona msimu huu.
Ili kujiweka pazuri kukimu mahitaji ya kimsingi ya wachezaji na waajiriwa wao, pamoja na kujiendeshea shughuli za kawaida muhula ujao, Barcelona wamepania kuwatia mnadani jumla ya wachezaji sita.
Kati yao ni Umtiti, Ivan Rakitic anayehusishwa na Inter Milan na Antoine Griezmann anayehemewa sana na Chelsea. Kiungo wao mwingine, Philippe Coutinho, ambaye kwa sasa anachezea Bayern Munich kwa mkopo huenda akatua Manchester United baada ya Bayern na Liverpool kumkataa.
Iwapo Arsenal au Man-United watashindwa pia kumudu bei ya Umtiti licha ya kupunguzwa kwa zaidi ya asilimia 50, basi Barcelona wamefichua azma ya kumtumia beki huyo kama chambo cha kujinasia mvamizi Lautao Martinez wa Inter Milan.
Hata hivyo, gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania limeshikilia kwamba Umtiti yuko radhi zaidi kunogesha soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) badala ya ile ya Italia (Serie A).
Umtiti ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Ufaransa kilichonyakua ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi, amekuwa mwepesi sana wa kupata majeraha ya kumweka mkekani kwa muda mrefu chini ya kipindi cha misimu miwili iliyopita.
Hadi kufikia mwisho wa msimu uliopita wa 2018-19, Umtiti alikuwa amewajibishwa na Barcelona katika michuano 11 pekee.
Makocha Ole Gunnar Solskjaer na Mikel Arteta wa Man-United na Arsenal mtawalia wanawania maarifa ya beki wa haiba kubwa katika juhudi za kuimarisha safu za ulinzi za vikosi vyao.
Iwapo Man-United watamkosa Umtiti ambaye ni shabiki wa tangu utotoni wa Arsenal, nyota wao wa zamani Rio Ferdinand amewataka kuziendea huduma za nyota wa Napoli na timu ya taifa ya Senegal, Kalidou Koulibaly kisha wamsajili Jadon Sancho wa Borussia Dortmund na Saul Niguez wa Atletico Madrid.