Bayern Munich waingia fainali ya German Cup
Na CHRIS ADUNGO
MABINGWA watetezi Bayern Munich walipiga Eintracht Frankfurt 2-1 na kufuzu kwa fainali ya German Cup ambayo kwa sasa itawakutanisha na Bayer Leverkusen.
Leverkusen walijikatia tiketi ya fainali ya German Cup baada ya kuwazamisha limbukeni Saabrucken 3-0 kwenye nusu-fainali ya kwanza.
Fainali itasakatiwa ugani Berlin Olympic mnamo Julai 4, 2020.
Bao la Ivan Perisic kunako dakika ya 14 ndilo lililokuwa la pekee hadi kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza katika kipute kilichotawaliwa na Bayern dhidi ya Frankfurt uwanjani Allianz Arena.
Mbali na kufukuzia taji la German Cup, Bayern ambao kwa sasa wananolewa na kocha Hansi Flick pia wanawania ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na wanahitaji alama sita pekee katika jumla ya mechi nne zijazo ili kutawazwa washindi wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa mara ya nane mfululizo.
Miamba hao wa soka ya Ujerumani kwa sasa wanajivunia kusajili ushindi katika jumla ya mechi 20 kutokana na 21 zilizopita katika mapambano yote.
Frankfurt ambao walitawazwa mabingwa wa German Cup mnamo 2018 walirejeshwa mchezoni kunako dakika ya 69 kupitia bao la Danny da Costa aliyecheka na nyavu muda mfupi baada ya kutokea benchi.
Mshambuliaji Robert Lewandowski aliwafungia Bayern bao la ushindi kunako dakika ya 74 baada ya kushirikiana vilivyo na kiungo Joshua Kimmich. Awali, bao la nahodha huyo wa timu ya taifa ya Poland lilikuwa limekataliwa na refa kwa madai kuwa alikuwa ameotea kabla ya kuhesabiwa baada ya kurejelewa kwa video ya teknolojia ya VAR.
Bao la Lewandowski lilikuwa lake la 45 kutokana na jumla ya mechi 39 ambazo amechezea Bayern hadi kufikia sasa msimu huu.