Chebet avizia rekodi ya dunia ya mita 5,000 Diamond League ya Zurich
BINGWA wa Olimpiki mbio za mita 5,000 na 10,000, Beatrice Chebet huenda akaandikisha historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza kukamilisha 5,000m chini ya dakika 14.
Ametangaza kuwa atavizia rekodi ya dunia ya mizunguko hiyo 12 na nusu kwenye fainali ya riadha za Diamond League mjini Zurich nchini Uswizi mnamo Septemba 5, 2024 saa nne kasoro dakika 17 usiku.
Chebet ametimka mita 5,000 kwa muda wake bora mwaka huu dakika 14:26.98, ingawa anajivunia muda bora wa 14:05.92 katika umbali huo alioandikisha mjini Eugene nchini Amerika mnamo Septemba 17, 2023.
Mkimbiaji huyo mwenye umri wa miaka 24 sasa anamezea mate rekodi ya dunia ya Muethiopia Gudaf Tsegay ya 14:00.21.
Tsegay alifyatuka rekodi hiyo akinyakua taji la Eugene Diamond League nchini Amerika mnamo Septemba 17, 2023.
Alifuta rekodi ya Mkenya Faith Kipyegon ya 14:05.20 iliyokuwa imedumu kwa miezi mitatu tu.
Chebet anashikilia rekodi ya dunia katika umbali wa 10,000m baada ya kukimbia 28:54.14 mjini Eugene mnamo Mei 25, 2024. Alivunja rekodi ya Muethiopia Letesenbet Gidey ya 29:01.03 iliyokuwa imara tangu Juni 8, 2021.
Vilevile, Chebet ndiye mshikilizi wa rekodi ya dunia ya kilomita tano barabarani ya wanawake pekee baada ya kutawala mashindano ya Cursa dels Nassos mjini Barcelona, Uhispania kwa dakika 14:13 mnamo Desemba 31, 2023.
Chebet atasaidiwa na teknolojia ya kutumia mwangaza katika juhudi zake za kuvizia rekodi ya dunia atakapoendea taji la Zurich dhidi ya wapinzani matata wakiwemo Waethiopia Tsigie Gebreselama (14:18.76) na Ejgayehu Taye (14:12.98).
“Nimetoka mbali katika safari yangu ya utimkaji na nimekuwa nikiimarika polepole,” akasema Chebet.
Aliongeza, “Kila mara nimejiambia kuwa sina haraka ya kutafuta matokeo mazuri. Lengo langu ni kuendelea kushinda na kuvunja rekodi moja baada ya nyingine na kujitafutia umaarufu kama mkimbiaji wa mbio za masafa marefu.”
Wakenya wengine katika fainali mjini Zurich ni Margaret Akidor (5,000m), Cornelius Kemboi, Jacob Krop na Daniel Munguti (3,000m), bingwa wa dunia Mary Moraa (800m), mfalme wa Afrika Julius Yego (kurusha mkuki), pamoja na Boaz Kiprugut, Reynold Cheruiyot na bingwa wa dunia mwaka 2019 Timothy Cheruiyot (1,500m).