Deni la Sh383 milioni, akaunti 16 FKF, ukaguzi wafichua
MASWALI yameibuka baada ya ripoti ya ukaguzi jana kufichua kuwa uliokuwa uongozi wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) uliacha deni la Sh383 milioni.
Ukaguzi uliofanywa na kamati ya mpito ya FKF ilifichua deni hilo pamoja na maovu mengine ambayo yalikuwa yakiendelea kwenye shirikisho chini ya utawala wa zamani.
Utawala uliopita wa FKF uliongozwa na Nick Mwendwa kama rais, Doris Petra kama naibu wake kisha Barry Otieno kama katibu wa shirikisho.
Waliondoka uongozini baada ya kubwagwa na rais wa sasa Hussein Mohamed kwenye uchaguzi ambao ulifanyika mnamo Disemba 7.
“Kufikia Disemba 31, 2024 FKF ilikuwa na deni la Sh383, 940, 846.70. Hii inajumuisha madeni kutoka wawasilishaji bidhaa, hali ambayo inaweka shirikisho kwenye hatari,” ikasema ripoti hiyo iliyowasilishwa kwa Mohamed mnamo Jumatano katika Hoteli ya Weston.
Kamati hiyo iliongozawa na Makamu wa rais wa FKF MacDonald Mariga, Mwakilishi wa Wanawake Kerubo Momanyi ambao walihudumu kama mwenyekiti na naibu mwenyekiti mtawalia.
Wanachama wengine walikuwa wakuu wa Baraza Kuu la FKF Charles Njoka (Mashariki) ambaye pia alikuwa katibu kisha Bernard Lagat (Kaskazini mwa Bonde la Ufa), Robert Macharia (Kati), Ahmedqadar Mohamed Dabar (Kaskazini Mashariki) na Peter ‘Kass Kass’ Kamau (Kati mwa Bonde la Ufa) pia wakishiriki.
Kamati hiyo pia ilipata kuwa FKF ina akaunti 16 za benki, hali ambayo inazua maswali kuhusu uwazi. Pia FKF inakabiliwa na changamoto tele za kisheria, ikiwa na kesi 21 zinazoiandama mahakamani.
“Haya yanajumuisha mizozo kuhusu chaguzi zilizopita, pesa za uwakili ambazo hazijalipwa na masuala mengine yanayohusiana na kandarasi,” akaongeza Mohamed.
Kamati hiyo ilipendekeza FKF iunganishe akaunti zake, isake njia muafaka ya kuyalipa madeni yake na kuongeza mgao wa pesa ambazo zinaelekezwa kwenye soka ya wanawake.
Wakati huo huo, Patrick Korir jana alijiondoa kama Katibu wa FKF baada ya kukaimisha kwenye wadhifa huo tangu Oktoba mwaka jana. Alichukua nafasi hiyo kutoka Barry Otieno ambaye alijiuzulu ili kuwania urais wa FKF.