Michezo

EPL: Breki kwa Liverpool Etihad

January 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

MANCHESTER, Uingereza

MANCHESTER, Uingereza: Pep Guardiola alivulia kofia nyota wake wa Manchester City kwa kuonyesha ujasiri mkubwa kwa kuvunja rekodi ya viongozi Liverpool kutoshindwa kwa kuwabwaga 2-1 na kuweka hai matumaini yao ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu.

Vijana wa Guardiola walikuwa na ulazima wa kushinda mchuano huo wa randi ya 21 kwa sababu kichapo kingeshuhudia Liverpool ikifungua mwanya wa alama 10 dhidi yao na kuwaweka katika hatari zaidi ya kuacha taji waliloshinda kwa rekodi ya alama 100 msimu uliopita.

Hata hivyo, walikuwa na ujasiri wa kutisha na kucharaza Liverpool kwa mara ya kwanza katika mechi tano kupitia kombora safi kutoka kwa Leroy Sane katika kipindi cha pili.

Sergio Aguero alifungua ukurasa wa magoli alipoweka wenyeji City kifua mbele dakika ya 40 na ingawa, Roberto Firmino alisawazisha dakika ya 64, City ilisalia tulivu na kwa ujasiri, haikupoteza mwelekeo wake na kumfanya Guardiola alimiminie sifa tele baada ya kipenga cha mwisho.

“Naona fahari katika kikosi hiki. Tulifahamu mechi hii ilikuwa fainali, tukiipoteza mambo yetu yatakuwa magumu zaid,” alisema Guardiola.

“Sifa zote zinawaendea wachezaji hawa ambao hawana kifani. Tulikuwa na shinikizo, lakini hatukuwa na uoga, hatukuogopa.

“Tulilemea timu kali. Tulikuwa sawa kutoka dakika ya kwanza.

“Liverpool hawafungwi mabao, na tulichana nyavu mara mbili. Tulisakata soka kwa ujasiri, tukiwania mipira na kubana wapinzani wetu.

“Tunafurahia ushindi huu kupunguza mwanya kati yetu na Liverpool. Kila kitu sasa kiko wazi.”

Guardiola alimiminia Aguero sifa za kipekee baada ya mshambuliaji huyu wa Argentina kupachika bao lake la 250 ligini kupitia shuti murwa kabla ya mapumziko.

Mfungaji huyu wa mabao mengi katika historia ya City sasa ameona lango katika mechi zake zote saba za nyumbani dhidi ya Liverpool.

“Tunahitaji Sergio Aguero katika mechi hizi, ufundi wake huleta tofauti kubwa,” alisema Guardiola.

“Kushinda mechi kama hizi, amefanya yote katika muda wake na mbinu aliyotumia kupata bao hilo ilikuwa ya kipekee.”

Akifahamu kipigo kingeweka mabingwa watetezi katika hatari zaidi, Guardiola aliomba wachezaji wake kutumia ushindi huu kama kichocheo cha kuongezea Liverpool presha.

“Sasa tuko alama nne nyuma yao na wao ndio viongozi. Lazima tuendelee kupigania kila pointi, lakini ushindi huu unatupa imani zaidi,” alisema.

“Tulifahamu kwamba tukishinda tutajirejesha katika vita vya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu, tukipoteza mambo yetu kwisha.

“Sikumbuki ligi kali kama hii, kuna orodha ndefu ya wagombeaji wa taji. Vita ni vikali, kila mechi ni kama fainali.” Liverpool itazuru uwanjani Amex kumenyana na Brighton katika mechi yake ijayo ya ligi Januari 12 nayo City itaalika Wolverhampton Wanderers uwanjani Etihad siku mbili baadaye.

Liverpool itaanza mechi dhidi ya Brighton na rekodi nzuri ya kuishinda mara tano mfululizo katika mechi timu hizi zimekutana. Wolves haijashinda City katika mechi tano zilizopita, ingawa mshindi hakupatikana katika mechi mbili zilizopita.