Michezo

FKF: Hatutaongezea KPL kandarasi ya kuendesha ligi 2020

May 26th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Soka la Kenya (FKF) halitaongeza kandarasi ya kampuni inayoendesha Ligi Kuu ya Kenya, KPL, itakapotamatika Septemba mwaka 2020.

Kwa mujibu wa tovuti ya redio ya Capital FM nchini Kenya, Rais wa FKF Nick Mwendwa alitangaza hayo baada ya Jopo la Kutatua mizozo ya michezo (SDT) kuionya FKF dhidi ya kuingilia majukumu ya KPL ya kuendesha ligi.

“Kandarasi hii inafikia tamati mwaka 2020. Ilisainiwa na afisi iliyotutangulia na hakuna chochote tunaweza kufanya. Kampuni ya KPL inahisi kwamba haitaki kusaidia timu ya taifa.

Kandarasi hii itakamilika Septemba mwaka 2020 na pengine kutoka hapo tutatimiza yale tunataka. Kabla ya tarehe hiyo, tutaendelea tu kuvutana nao. Hatuna mipango ya kuruhusu shirika lingine kuendesha ligi tena,” Mwendwa aliapa.

Mwaka 2016, FKF na KPL zilivutana kuhusu idadi ya klabu za Ligi Kuu. Mwendwa na FKF walipigania kuona washiriki wakiongezeka hadi 18 kutoka 16 nayo KPL ilitaka ligi hiyo isalie na klabu 16. Baada ya vuta-nikuvute, ligi ya klabu 18 ilianza kusakatwa mwaka 2017.

Kampuni ya KPL ilizaliwa mwaka 2003 ili kutatua migogoro ya mara kwa mara ya viongozi katika shirikisho iliyochangia kuzorota kwa viwango vya soka nchini.

Klabu ziliamua kuanzisha kampuni itakayoendesha ligi kwa uwazi na bila matatizo. Wamiliki wa kampuni hii ni klabu zinazoshiriki Ligi Kuu. Afisa Mkuu Mtendaji wa KPL ni Jack Oguda naye Frank Okoth ni Afisa Mkuu wa Mipango.