FKF ilipata Sh7m katika mechi ya Gabon na Stars
RAIS wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) Hussein Mohamed Jumanne alitangaza kuwa walikusanya takriban Sh7 milioni kupitia ada za kiingilio wakati wa mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 kati ya Harambee Stars na Gabon mnamo Jumapili.
Mchuano huo ambao ulihudhuriwa na halaiki ya mashabiki, uligaragazwa katika uga wa Nyayo ambao una uwezo wa kuwasitiri mashabiki 22,000. Gabon ilishinda Kenya 2-1 katika mchuano huo wa Kundi E.
Mohamed aliwashukuru mashabiki kwa kufika katika uga huo kwa wingi japo akakiri kutotimizwa viwango vya juu vya usalama kulisababisha msongamano na msukumano uliosababisha lango moja la Nyayo kuvunjwa.
“Tuliuza tikiti 15,968 za eneo la kawaida, tikiti 1,331 za wageni mashuhuri kisha maegesho yalikuwa na tikiti 239. Eneo la wageni mashuhuri zaidi na waalikwa lilikuwa na tikiti 17,735.
Hata hivyo, kuna tikiti kidogo zilizobaki lakini kwa jumla pesa ambazo tulikusanya zilikuwa Sh6,998, 497,” akasema Mohamed.
Ilikuwa mechi ya kwanza kwa Harambee Stars kucheza nyumbani baada ya miaka miwili. Mohamed alisema maandalizi hayakufikia viwango au matarajio ya wengi na mechi zijazo watajitahidi kufanya vyema zaidi.
Kuhusu kukomesha tabia ya mashabiki kuvamia uwanja na fujo zilizoshuhudiwa langoni, Mohamed alisema shirikisho litaendeleza mafunzo ili Wakenya wawe na ustaarabu kwenye mechi zijazo.
Mohamed pia alikanusha vikali madai kuwa tikiti zilikuwa zikiuzwa au kunadiwa kwa manufaa ya kifedha ya watu wachache akisema hawajapata ushahidi wowote wa kuthibitisha tukio kama hilo.
Hata hivyo, aliibua wasiwasi kuhusu iwapo mechi za kimataifa bado zitaandaliwa Nyayo akisema jinsi uwanja huo ulivyojengwa, kuhakikisha mikakati yote ya usalama inatimizwa ni kibarua mno ikiwa mashabiki wamejazana.
Mohamed alipendekeza mechi za hadhi kama hizo ziwe zikiandaliwa katika uga wa kimataifa wa Kasarani ambao bado unaendelea kufanyiwa ukarabati.
Mwenyekiti wa Kamati Andalizi ya Mashindano ya Soka Afrika kwa Wachezaji wanaoshiriki Ligi ya Nyumbani (CHAN) Nicholas Musonye aliwashukuru mashabiki kwa kufurika Nyayo lakini akasema hawakuwa na nidhamu kwa kuvamia uwanja.
“Suala la usalama na kile kilichotokea kabla na baada ya mechi ni masuala ya kusikitisha mno. Uwanja huu bado unajengwa na sasa tunamakinikia kuweka vizuizi kuwazuia mashabiki kuingia uwanjani baada ya mchezo,” akasema Musonye , Katibu wa zamani wa CECAFA.