Gor, Police, Murangá Seal na Mara Sugar kutifuana Mozzart Bet leo
CHINI ya Kocha mshikilizi Zedekiah ‘Zico’ Otieno, Gor Mahia itakuwa inalenga kuendeleza juhudi za kutwaa Kombe la Mozzart Bet leo huku nafasi ya kushinda taji la Ligi Kuu (KPL) ikionekana kuendelea kuwa finyu na haipo mikononi mwao.
Gor itavaana na Murang’a Seal kwenye mechi ya nusu fainali katika uga wa Dandora kuanzia saa 10 jioni. Mechi hiyo itatanguliwa na ile ya robo fainali kati ya Kenya Police na Mara Sugar katika uga huo huo kuanzia saa saba mchana.
Mshindi wa mechi kati ya Gor na Murang’a Seal atafuzu fainali ya Mozzart Bet kwenye tarehe ambayo itatangazwa na Shirikisho la Soka Nchini (FKF) mwezi ujao.
Nairobi United ambayo ilifuzu nusu fainali kwa kubandua Kakamega Homeboyz 2-0 hawatakuwa wakiwajibikia leo. Hii ni kwa sababu vijana wa kocha Nicholas Muyoti bado wanasubiri mshindi kati ya Kenya Police na Mara Sugar.
Wasaga miwa hao walipiga Compel 2-0 katika raundi ya 16 Jumatano kwenye uga wa Jomo Kenyatta Kisumu na wakajipatia tikiti ya kukutana na Kenya Police.
Mechi hiyo ya raundi ya 16 haikuchezwa jinsi ambavyo ilikuwa imeratibiwa kutokana na kesi ambayo iliwasilishwa na AFC Leopards. Ingwe iliwasilisha rufaa baada ya Kamati ya Mashindano Ligini kutoa uamuzi ambao uliwapa Mara Sugar ushindi kwenye mechi ya raundi ya 32 mnamo Machi 8.
Katika mechi hiyo uwanja wa Jomo Kenyatta, mashabiki wa Leopards walivamia uwanja baada ya refa kubadilisha uamuzi wa kuwapa penalti dakika ya 89.
Ingwe ilipinga uamuzi wa kuwapa Mara Sugar ushindi lakini ikapoteza kwenye rufaa hiyo ambayo uamuzi wake ulitolewa Mei 8.
Mshindi wa Kombe la Mozzart Bet atawakilisha nchi katika Kombe la Mashirikisho Afrika (Caf). Mashindano haya ni mwanya mwingine wa Gor kuendelea kushiriki soka ya Afrika hata wakipoteza taji la KPL kwa Kenya Police.
“Tunajua kile ambacho kiko mbele yetu na tunamakinika kuyarekebisha makosa ambayo tulifanya dhidi ya Murang’a Seal wikendi iliyopita. Nia yetu ni kufika fainali kisha kubeba taji hili,” akasema Kiungo wa Gor Enock Morrison kuelekea mchuano huo.
Wikendi iliyopita, Murang’a Seal ilikuwa mwenyeji wa Gor na timu hizo zikatoka sare tasa uga wa Sportpesa Arena jijini Murang’a.
“Mechi yetu dhidi yao wikendi iliyopita haikuwa rahisi, tulijifunza kutokana na mchezo wao na tutatumia mbinu mpya kuhakikisha tunawashinda. Kila mtu yuko sawa hata baada ya kocha wetu kuondoka na sisi tunatarajia kupata ushindi,” akasema Kiungo wa Gor Lawrence Juma.
Gor haijawahi kupoteza kwa Murang’a Seal tangu timu hiyo inayonolewa na Yusuf Chipo ipandishwe KPL mnamo 2023. Wameshinda mara moja na mechi nyingine tatu zimeishia sare.