Gor yanyanyaswa na wanyonge FC Talanta Dandora
MBIO za Gor Mahia za kupigania ubingwa wa Ligi Kuu (KPL) msimu wa 2024/25 Alhamisi zilipata pigo baada ya kutandikwa 1-0 na FC Talanta katika uga wa Dandora, Nairobi.
Bao la pekee lilifungwa na Emmanuel Osoro katika kipindi cha kwanza baada ya kuwahi shuti kali ndani ya kijisanduku kutoka kwa Cliff Oruko. FC Talanta waliongozwa kwenye mechi hiyo na naibu kocha Jackson Gatheru kwa kuwa Jackline Juma, kocha pekee wa kike KPL, hakuwepo.
Katika dakika ya 80, Gor ilikuwa na nafasi ya kusawazisha bao hilo lakini mpira wa ikabu uliopigwa na kiungo Austin Odhiambo ulipiga mtambapanya. Naibu Kocha Zedekiah ‘Zico’ Otieno aliongoza K’Ogalo katika ngarambe hiyo japo hakuwa mazoezini na timu Jumatu na Jumanne.
Kocha wa Gor Sinisa Mihic aliketi eneo la mashabiki kwa kuwa anatumikia marufuku ya mechi mbili baada ya kulishwa kadi nyekundu katika ushindi wa 1-0 dhidi ya KCB mnamo Aprili 1.
Hii ilikuwa mara sita K’Ogalo ilikuwa ikipoteza msimu huu na sasa wana kibarua kikali kutetea taji lao. Baada ya mechi 27 na zikiwa zimesalia mechi saba msimu umalizike, Gor imejizolea alama 47, alama nne nyuma ya viongozi Tusker.
Baadhi ya mashabiki wa Gor wamelalamikia matokeo duni ya klabu hiyo huku wakihusisha na vuta nikuvute na tofauti kali kati ya Mihic kwa upande moja kisha Otieno, Michael Nam na Meneja wa timu Victor Nyaoro.
“Kuwashinda mabingwa watetezi si rahisi lakini katika soka hakuna kisichowezekana. Hii ilikuwa siku yetu, tulicheza vizuri, tukapata alama zote na nimefurahi sana,” akasema Naibu kocha wa FC Talanta Jackson Gatheru.
FC Talanta wapo nafasi ya 14 kwa alama 29 baada ya mechi 28.
Otieno alikwepa mahojiano akionekana kuhofia ghadhabu za mashabiki waliokerwa na kichapo hicho