Gor yatinga fainali, Police wakiuma nje Kombe la Mozzart Bet
GOR MAHIA JUMAPILI ilijiweka pazuri kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu (KPL) na Kombe la Mozzart Bet huku Kenya Police ikibanduliwa kwenye mechi zilizochezwa uga wa Dandora, Nairobi.
K’Ogalo ilitinga fainali ya Mozzart Bet Cup baada ya kushinda Murangá Seal 5-4 kupitia mikwaju ya penalti. Hii ni baada ya timu hizo kuagana sare ya 2-2 katika muda wa kawaida.
Mabao ya Gor yalifungwa na Bryson Wangai na Alpha Onyango huku Austin Odhiambo akiwafungia penalti ya ushindi. Nao Murang’a Seal walifungiwa na Wilson Kamau na Michael Owen.
Kenya Police nao walipoteza 8-7 dhidi ya Mara Sugar kwenye mechi ya robo fainali katika mchuano ambao ulianza mapema uga huo huo wa Dandora. Timu hizo zilikuwa zimeagana sare ya 1-1 muda wa kawaida.
Mara Sugar ilikuwa imechukua uongozi kupitia Dennis Cheruiyot dakika ya nane lakini Kenya Police ikasawazisha dakika ya 30 kupitia Brian Okoth.
Kenya Police walibakia wachezaji 10 uwanjani dakika ya 76 baada ya beki David ‘Cheche’ Ochieng’ kupewa kadi ya pili ya njano kisha kadi nyekundu.
Kufuatia ushindi dhidi ya Seal, Gor sasa imetinga fainali ambapo itakutana na mshindi wa nusu fainali kati ya Nairobi United na Mara Sugar.
Nairobi chini ya Nicholas Muyoti ndiyo timu pekee ambayo si ya KPL ambayo imehimili na kutinga nusu fainali huku ikitoa vigogo Kakamega Homeboyz na Tusker.
Mshindi wa Mozzart Bet Cup huwakilisha taifa katika Kombe la Mashirikisho Afrika (CAF) pamoja na kutia kibindoni jumla ya Sh2 milioni.
Katika KPL, Kenya Police inahitaji ushindi moja tu kujihakikishia taji japo ina kibarua dhidi ya Shabana na Gor katika mechi mbili zilizosalia kabla ya msimu wa 2024/25 kutamatika.
Gor nao itavaana na AFC Leopards, Ulinzi Stars kisha Kenya Police ambapo ikishinda mechi hizo zote nao Kenya Police ipata sare au ipoteze dhidi ya Shabana, K’Ogalo itashinda ubingwa wake wa 22 wa KPL.
“Tumecheza vizuri, Seal walikuwa wapinzani wagumu na tulipiga vyema mikwaju yetu ya penalti. Kwa sasa la muhimu ni kushinda mechi zetu zote wala hakuna nafasi ya kudondosha hata alama moja,” akasema Kaimu kocha wa Gor Zedekiah ‘Zico’ Otieno.