HANG’OKI! Liverpool kurefusha mkataba wa Klopp
Na MASHIRIKA
MERSEYSIDE, UINGEREZA
LIVERPOOL wanalenga sasa kurefusha mkataba wa Jurgen Klopp baada ya mkufunzi huyo mzaliwa wa Ujerumani kuwaongoza kunyanyua ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.
Mkufunzi huyo kwa sasa hupokezwa mshahara wa hadi Sh980 milioni kwa mwaka uwanjani Anfield.
Kulingana na vinara wa Fenway Sports Group (FSG) ambao ni wamiliki wa Liverpool, kuongezwa kwa muda wa kuhudumu kwa Klopp uwanjani Anfield kwa miaka mingine mitatu kutawazima Bayern Munich na Barcelona ambao kwa sasa wanavizia maarifa ya kocha huyo.
Sawa na Barcelona ambao huenda wakachochewa kumtema mkufunzi Ernesto Valverde aliyeshindwa kuwanyanyulia ubingwa wa UEFA na Copa del Rey msimu huu, Bayern pia wamedokeza nia ya kuagana rasmi na kocha Niko Kovac kufikia Agosti 2019.
Zaidi ya mashabiki 750,000 walimlaki Klopp na wachezaji wake uwanjani Anfield, Uingereza mwishoni mwa wiki jana baada ya miamba hao wa soka kuwapepeta Tottenham Hotspur 2-0 katika fainali ya UEFA iliyoandaliwa katika uwanja wa Wanda Metropolitano jijini Madrid, Uhispania.
Klopp ambaye kandarasi yake ya sasa na Liverpool inatamatika mnamo 2022, pia aliwaongoza waajiri wake kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika nafasi ya pili kwa alama 97, moja pekee nyuma ya Manchester City walioweka historia ya kuwa kikosi cha pili baada ya Manchester United kuhifadhi ubingwa wa taji la EPL na pia kutia kibindoni jumla ya makombe matatu kwa mkupuo.
Liverpool walipoteza mchuano mmoja pekee (dhidi ya Man-City) katika jumla ya mechi 38 kwenye kampeni za EPL muhula huu.
Mbali na kutawazwa wafalme wa EPL, kocha Pep Guardiola pia aliwaongoza masogora wake kunyanyua ubingwa wa Carabao Cup na Kombe la FA kwa kuwatandika Chelsea na Watford mtawalia.
“Klopp ni kocha wa haiba kubwa ambaye anakijali sana kikosi. Amedhihirisha kwamba anatawaliwa na kiu ya kujihusisha na ushindi na pia kufanikisha kampeni za Liverpool kila msimu. Mchango wake kufikia sasa hauhitaji maelezo zaidi,” akatanguliza Mwenyekiti wa Liverpool, Tom Werner.
“Wachezaji wa Liverpool walipombeba Klopp juu kwa juu baada ya kunyanyua taji la UEFA, walikuwa wakionyesha jambo ambalo mashabiki wote wa kikosi hiki wanafahamu. Kwamba ni kocha ambaye ni kipenzi cha kila mchezaji na yeyote anayefurahishwa na soka safi,” akasema kinara huyo.
Kombe la kwanza
Ushindi dhidi ya Spurs katika UEFA uliwapa Liverpool kombe lao la kwanza tangu ujio wa Klopp ambaye alisajiliwa kutoka Borussia Dortmund nchini Ujerumani mnam 2015.
Klopp alikiri pia kuridhishwa na wingi wa mashabiki waliojitokeza kuwakaribisha uwanjani Anfield kabla ya sherehe zenye hekaheka na mbwembwe za kila sampuli kuhanikiza anga, vichochoro na barabara nyingi za jiji la Merseyside, Uingereza.
“Sijui kabisa jinsi watu wanavyoishi Liverpool. Sijui mengi kuhusu utamaduni na desturi zao. Lakini ambacho kimejidhihirisha ni kwamba hakuna nafasi kubwa kwa vikosi vingine vya soka ya bara Ulaya miongoni mwa mashabiki wa jiji hili,” akasema Klopp katika mahojiano yake na LFC TV.
“Inastaajabisha sana. Mtoto mdogo anayezaliwa leo hana kabisa klabu mbadala ya kujiteulia kuunga mkono na kushabikia isipokuwa Liverpool. Hii ina maana kubwa sana. Ni mojawapo ya mambo yanayochangia ufufuo wa kikosi hiki ambacho kimepania kuendeleza ubabe katika soka ya Ulaya,” akaongeza.
Liverpool ambao walizidiwa maarifa na Real Madrid kwenye fainali ya UEFA msimu jana, walisajili ushindi katika michuano tisa ya mwisho ya kampeni za EPL msimu huu.
Alama 97 walizojizolea ndizo za tatu kwa wingi zaidi katika historia ya kampeni za EPL. Pointi 100 ambazo Liverpool walitia kapuni msimu jana ndizo za juu zaidi kuzolewa na kikosi katika msimu mmoja wa kivumbi cha EPL huku alama 98 za msimu huu zikiwa ndizo za pili kwa wingi zaidi.