Michezo

Harambee Stars roho juu ikivaana na Gambia leo

Na CECIL ODONGO March 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KENYA italenga kumaliza ukame wa kutoshinda mechi za kufuzu Kombe la Dunia au Kombe la Afrika (AFCON) ugenini leo itakapovaana na Gambia kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026.

Mechi hiyo ya kundi F itagaragazwa katika uga wa Stade Alassane Quattara jijini Abidjan, Cote d’Ivoire. Itaanza saa nne usiku saa za Afrika Mashariki.
Gambia iliamua kuandaa mechi hiyo Cote d’Ivoire kutokana na ukosefu wa uga ambao umeidhinishwa na Shirikisho la Soka Duniani, FIFA na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Jumatatu wiki ijayo, Gambia itacheza na Cote d’Ivoire ambao ni mabingwa watetezi wa Afcon.

Hii itakuwa mechi ya kwanza kati ya Kenya na Gambia ambao hawajawahi kuonana hata kwenye mchezo wa kirafiki au mchuano wowote wenye ushindani.
Hata hivyo, itabidi Kenya iwe kwenye ubora wake ili kuwahi ushindi ugenini ambao umewakwepa hata kama wamekuwa wakifunga magoli.
Mara ya mwisho Harambee Stars iliposhinda mechi ya kufuzu Kombe la Dunia ni mnamo Oktoba 7, 2015 ilipolaza Mauritius mnamo 5-2.
Katika mechi za kufuzu Kombe la Afrika, ushindi wa mwisho wa Kenya ni mnamo Machi 29, 2021, ilipopiga Togo 2-1 jijini Lome.

Katika mechi ya mwisho ya ugenini ya kufuzu Kombe la Afrika ambayo Kenya ilicheza, Harambee Stars ilipigwa 4-1 na Cameroon mnamo Oktoba 11, 2024.
Katika mechi ya mwisho ya kufuzu Kombe la Dunia ugenini, Harambee Stars iliagana sare ya 1-1 na Burundi mnamo Juni 7, 2024.

Takwimu zinaonyesha kuwa Kenya imekuwa ikifunga katika mechi hizo za ugenini hata kama inachapwa. Kwenye msimamo wa viwango vya FIFA, Gambia inashikilia nambari 125 huku Kenya ikikamata nafasi ya 108.
Itakuwa mechi ya kwanza kwa kocha Benni McCarthy ambaye alichukua usukani kama kocha wa Harambee mnamo Machi 3.
Mwenzake wa Gambia Johnatha McKinstry naye amekuwa mamlakani kwa miaka miwili.

McKinstry aliifundisha Gor Mahia kati ya Julai 2022 hadi Mei 24, 2024 ambapo alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu (KPL) na ataungana na beki Rooney Onyango ambaye alifanya naye kazi kambini mwa K’Ogalo.
Nahodha wa Harambee, Michael Olunga amesema wanalenga kuwika katika mchuano huo na ana imani watapata ushindi.
“Tumejiandaa vizuri na nina imani tutapata ushindi ikizingatiwa pia tuna baadhi ya wachezaji wazuri wachanga katika kikosi chetu,” akasema Olunga.