Harambee Stars washuka viwango bora vya FIFA
TIMU ya taifa ya soka ya wanaume ya Kenya maarufu kama Harambee Stars, imeshuka kwenye viwango bora vipya vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mnamo Ijumaa, Aprili 4, 2025.
Vijana wa kocha Benni McCarthy wametupwa chini kutoka 108 duniani (Desemba 19, 2024) hadi 111 baada ya kutoka 3-3 na Gambia (Machi 20) na kupoteza 2-1 mikononi mwa Gabon (Machi 23) kwenye mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2026 za Kundi F.
Cote d’Ivoire wanaongoza kundi kwa alama 16 Ikifuatiwa na Gabon (15), Burundi (10), Kenya (sita), Gambia (nne) na Ushelisheli (sufuri) baada ya mechi sita za kwanza.
Morocco wanasalia namba wani Barani Afrika baada ya kuimarisha alama zao kwa 6.06 hadi 1,694.24.
Atlas Lions wanakamata nafasi ya 12. Wameruka juu nafasi mbili duniani.
Senegal ni nambari mbili Afrika na 19 duniani kwa alama 1,630.32 baada ya kupoteza alama 6.93.
Teranga Lions wameshuka nafasi mbili duniani.
Misri wameongeza alama 5.31 wakipaa nafasi moja duniani na kutulia nambari 32.
Mafirauni hao, ambao ni nambari tatu Afrika, wana jumla ya alama 1,518.
Algeria, Cote d’Ivoire, Nigeria na Tunisia wote wamepiga hatua mbele hadi nafasi ya nne, tano, sita na saba Barani Afrika, mtawalia.
Waalgeria wako juu nafasi moja hadi 36 duniani.
Les Elephants wa Cote d’Ivoire wamepaa nafasi tano na kutulia nafasi ya 41 duniani.
Super Eagles ya Nigeria inapatikana nafasi ya 43 duniani baada ya kuruka juu nafasi moja.
Watunisia wameruka kutoka 52 hadi 49 duniani.
Cameroon wanafunga 50-bora duniani katika nafasi ya nane Afrika baada ya kuteleza nafasi moja.
Kwa wapinzani Kenya katika Kundi F, Cote d’Ivoire wanaongoza wakifuatiwa na Gabon (wameimarika kutoka 84 hadi 79 duniani), Gambia (wameteremka nafasi moja hadi nambari 126 duniani), Burundi (wako chini nafasi moja hadi 140 duniani) na Ushelisheli (wanakamata nambari 203 kutoka 201).
Katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Uganda wako juu katika nafasi ya 89 duniani wakifuatiwa na Tanzania (wameshuka kutoka 106 hadi 107), Kenya (chini nafasi tatu hadi nambari 111 duniani), Sudan (wameshuka kutoka 113 hadi 114), Rwanda (wameporomoka kutoka 124 hadi 130), Burundi (wako chini kutoka 139 hadi 140), Ethiopia (wameanguka kutoka 146 hadi 147), Sudan Kusini (wamesalia 170), Djibouti (wako chini nafasi moja hadi 192) nao Eritrea hawajaorodheshwa kutokana na kuwa hawajakuwa wakisakata mechi.
Viwango bora vijavyo vitatangazwa Julai 10, 2025.