Michezo

Harambee stars yaumiza nyasi bure huko Uganda

Na GEOFFREY ANENE September 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

TIMU ya taifa ya Kenya, Harambee Stars iliambulia alama moja baada ya kuanza safari ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2025 kwa kuumiza nyasi bure katika sare tasa ugani Mandela nchini Uganda mnamo Ijumaa, Septemba 6, 2024.

Vijana wa kocha Engin Firat walilenga shuti moja pekee kwenye lango na kupiga fyongo makombora manne katika mechi hiyo waliyomiliki mpira kwa asilimia 51 na kupata kona tano dhidi ya Wazimbabwe katika mchuano huo wa Kundi J.

Ajabu ni kuwa Firat aliamua kutumia beki Joseph Okumu (Reims, Ufaransa) katika safu ya mashambulizi katika mfumo wa 4-3-3.

Nahodha Okumu almaarufu Crouch, alishirikiana na viungo Austine Odhiambo Otieno (Gor Mahia) na Eric Johana Omondi (Uta Arad, Romania) katika safu ya mashambulizi.

Kwa kufanya hivyo, Mturuki Firat alionyesha hana imani sana na washambulizi Jonah Ayunga (St. Mirren, Scotland), Victor Omune (AFC Leopards), John Avire (Sekka El Hadid, Misri), Benson Omala (Safa, Lebanon) na Alwyn Tera (FC Ararat, Armenia) kwani aliwaanzisha kitini, huku mfumaji matata Michael Olunga akiendelea kuuguza jeraha.

Firat aliingiza Amos Nondi katika nafasi ya Alphonce Omija dakika ya 21, John Avire katika nafasi ya Omondi katika dakika ya 68, Tera katika nafasi ya Duke Abuya dakika ya 86 na Abud Omar katika nafasi ya Eric Ouma,

Kenya, ambayo imekosa makala mawili mfululizo ya AFCON, itakabana koo na Namibia nchini Afrika Kusini mnamo Septemba 10 katika mechi ya pili. Kundi hilo pia liko na mabingwa mara tano wa Afrika, Cameroon.

Timu mbili za kwanza kutoka kundi hili ndizo zitaingia AFCON 2025 nchini Morocco moja kwa moja.

Wachezaji wa kikosi cha kwanza cha 11 wa Harambee Stars walikuwa :

Kipa – Byrne Omondi (Bandari FC);

Mabeki – Joseph Stanley Okumu (nahodha/Reims – Ufaransa), Sylvester Owino Ahono (Gor Mahia), Alphonce Otieno Omija (Gor Mahia), Erick Ouma Otieno (Rakow, Poland);

Viungo – Anthony Akumu Agay (Kheybar, Iran), Austine Odhiambo Otieno (Gor Mahia), Duke Ooga Abuya (Yanga SC, Tanzania), Richard Odada (Dundee United, Scotland), Ronney Otieno Onyango (Gor Mahia), Eric Johana Omondi (Uta Arad, Romania).

Wachezaji wa akiba nao walikuwa:

Kipa – Levis Opiyo (AFC Leopards), Patrick Matasi (Kenya Police);

Mabeki – Abud Omar (Kenya Police), Amos Nondi (FC Ararat, Armenia), Sharif Majabe (Bandari FC);

Viungo – Kenneth Muguna (Kenya Police), Chrispine Erambo (Tusker);

Washambulizi – Jonah Ayunga (St. Mirren, Scotland), Victor Omune (AFC Leopards), John Avire (Sekka El Hadid, Misri), Benson Omala (Safa, Lebanon) na Alwyn Tera (FC Ararat, Armenia);