Harry Kane alenga kufunga jumla ya mabao 200 katika EPL na kufikia rekodi za Shearer na Rooney
Na CHRIS ADUNGO
MSHAMBULIAJI matata wa Tottenham Hotspur, Harry Kane amesema kwamba analenga kuwa mchezaji wa tatu baada ya Alan Shearer na Wayne Rooney kufunga jumla ya mabao 200 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Mnamo Juni 23, 2020, Kane alifunga goli katika ushindi wa 2-0 uliosajiliwa na Tottenham dhidi ya West Ham United katika kipute cha EPL. Bao hilo lilikuwa la 137 kwa Kane kufunga katika jumla ya mechi 200 ambazo amewachezea Tottenham.
Hadi kufikia sasa, ni Shearer pekee na Rooney ndio wanajivunia kupachika wavuni zaidi ya mabao 200 katika historia ya soka ya EPL.
“Bado nina umri wa miaka 26 pekee. Ni matarajio yangu kwamba nitarejea katika hali shwari hivi karibuni na kuanza kufunga mabao zaidi. Hakuna kitu cha tija chenye fahari kubwa zaidi kwa mwanasoka yeyote kuliko kufunga mabao,” akatanguliza Kane.
“Siamini kwamba nimefikisha mechi 200 tayari. Miaka kwa kweli inasonga na italazimu nijikakamue zaidi msimu ujao ndipo niweke hai matumaini ya kufikia malengo yangu,” akasema Kane.
Hadi alipofunga dhidi ya West Ham, mara ya mwisho kwa Kane kutikisa nyavu za wapinzani ilikuwa mnamo Disemba 2019. Baada ya mechi hiyo, alipata jeraha baya lililomweka nje kwa kipindi cha miezi sita. Kufikia sasa, anajivunia jumla ya mabao 12 msimu huu.
Kwa sasa, Sergio Aguero ndiye anayejivunia idadi kubwa zaidi ya mabao katika soka ya Uingereza. Sogora huyo wa Manchester City na timu ya taifa ya Argentina amefunga magoli 138, moja zaidi kuliko Kane.
Aliyekuwa mshambuliaji wa Arsenal, Thierry Henry alipachika wavuni jumla ya mabao 131 kutokana na michuano yake 200 ya kwanza kambini mwa The Gunners.
Kane ndiye mchezaji wa 11 kuwahi kuwajibishwa na Tottenham katika jumla ya mechi 200. Wengineo ni Sol Campbell, Teddy Sheringham, Robbie Keane, Jermain Defoe na Christian Eriksen aliyejiunga na Inter Milan mwanzoni mwa msimu huu.
Bao la Kane dhidi ya West Ham lilikuwa lake la tisa dhidi ya kikosi hicho. Sogora huyo anayemezewa mate na Man-United na Real Madrid anakuwa mchezaji wan ne baada ya Henry, Sheringham na Frank Lampard kuwahi kufunga angalau mabao 30 kwenye debi za jiji la London.
Na iwapo atafaulu kufikisha jumla ya mabao 200 kapuni mwake kutokana na mechi za EPL, Kane atakuwa mchezaji wa tatu baada ya Shearer (260) na Rooney (208) kufikia ufanisi huo.
Shearer alifikisha idadi hiyo ya mabao kutokana na mechi 441 huku rekodi ya Rooney ikija baada ya kusakata jumla ya mechi 491.