Michezo

HOFU KUU! Hofu ya coronavirus yalazimu Man-United kumtenga Ighalo

February 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

KLABU ya Manchester United imefichua kuwa, sajili mpya Odion Ighalo anafanya mazoezi mbali na wenzake kama tahadhari dhidi ya homa hatari ya Coronavirus, baada yake kuwasili kutoka China ambako kunashuhudiwa mkurupuko wa homa hiyo.

Man-United imeamua kuchukua hatua hiyo kwa sababu ya hatari, japo kidogo, ya maambukizi ya homa hiyo inayosababishwa na virusi vya Corona.

Homa hiyo iliyojitokeza Desemba mwaka jana imesababisha vifo vya watu zaidi ya 1,350 nchini China na wawili nje ya taifa hilo, kufikia sasa.

Vile vile, kumekuwa na jumla ya maambukizi 60,000 ndani na nje ya taifa hilo.

Mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) waliamua kutosafiri na straika Ighalo nchini Uhispania kwa kambi ya mazoezi wakati wa likizo fupi ya majira ya baridi, kwa sababu ya hofu kwamba yaweza kuwa vigumu kuruhusiwa kurejea nchini Uingereza.

Tahadhari ya kiafya inasema kuwa wasafiri wanaoingia Uingereza kutoka nchi fulani, ikiwemo China, wanajitenga na watu kwa siku 14 ili kuzuia uenezaji wa maradhi hayo hatari.

Raia huyo wa Nigeria ambaye zamani aliichezea Watford, anatarajiwa kujumuishwa kwenye kikosi cha Man-United kitakachocheza ugenini dhidi ya Chelsea, katika mechi ya Jumatatu usiku.

Taarifa zinasema Ighalo, 30, amekuwa akifanya mazoezi akifuata ratiba mahususi ya klabu hiyo ili kuwa tayari kwa mechi hiyo ya Ligi Kuu.

Anaendelea na mazoezi hayo katika ukumbi wa kitaifa wa mchezo wa taekwondo, National Taekwondo Centre ulio karibu na ambako amekuwa akiishi tangu awasili Uingereza siku 11 zilizopita.

Ighalo amejiunga na United kwa mkopo hadi mwisho wa msimu kutoka klabu ya Shanghai Shenhua inayoshiriki Ligi Kuu ya China.

Mashindano mengi ya michezo yamefutiliwa mbali nchini China na mataifa ya Mashariki ya Mbali, ikiwemo mbio za magari ya langalanga almaarufu Formula 1, mkondo wa Chinese Grand Prix.

Wakati huo huo, mwenyekiti wa zamani wa Crystal Palace, Simon Jordan ameomba Man-United isimpe kocha Ole Gunnar Solskjaer fedha zaidi za kununua wachezaji.

Anataka klabu hiyo iwazie kwa makini akidai kocha huyo raia wa Norway ametumia fedha nyingi lakini hakuna matokeo mazuri uwanjani.

Man-United ilinunua Bruno Fernandes kutoka Sporting Lisbon kwa ada ya Sh6 bilioni mwezi uliopita, kabla ya kumpata Ighalo kwa mkopo.

Katika kipindi kirefu cha uhamisho cha mwaka 2019, Solskjaer alipewa Sh13 bilioni kupata huduma za Daniel James, Aaron Wan-Bissaka na Harry Maguire.

Wachezaji hao watatu wamekuwa moto-baridi huku Man-United wakishikilia nafasi ya nane ligini kwa alama 35, baada ya kusakata mechi 25.