Michezo

Icardi apokezwa mkataba wa kudumu kambini mwa PSG

May 31st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

MIAMBA wa soka ya Ufaransa, Paris Saint-Germain (PSG) wamemsajili mshambuliaji matata wa Inter Milan na timu ya taifa ya Argentina, Mauro Icardi kwa kima cha Sh7.5 bilioni.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 aljiunga na PSG kwa mkopo wa msimu mmoja mnamo Septemba 2019.

Kwa mujibu wa mkataba mpya alioutia saini kambini mwa PSG chini ya uangalizi wa wakala na mke wake, Wanda Nara, mfumaji huyo kwa sasa atahudumu ugani Parc des Princes hadi mwishoni mwa Juni 2024.

Icardi alipachika wavuni jumla ya mabao 20 kutokana na mechi 31 alizowachezea PSG katika mapambano yote kabla ya soka ya Ufaransa kutamatishwa rasmi kwa sababu ya corona mnamo Aprili 30 huku zikisalia mechi 10 kwa muhula huu kukamilika.

Icardi amekuwa akiwania nafasi katika kikosi cha kwanza cha PSG kwa pamoja na fowadi mkongwe wa Uruguay, Edinson Cavani.

Mkataba wa Cavani ambaye ni mfungaji bora wa muda wote ugani Parc des Princes unatamatika rasmi Juni 30.

“FC Internazionale Milano inatangaza uhamisho wa Mauro Icardi ambaye sasa ameingia katika sajili rasmi ya PSG. Klabu inamshukuru Icardi kwa kipindi cha miaka sita ambayo amehudumu ugani San Siro,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Inter ambao wanashiriki Ligi Kuu ya Italia (Serie A).