Michezo

IKO SHIDA: Jeraha la Mohamed Salah laikosesha Liverpool usingizi

November 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MERSEYDE, Uingereza

KLABU ya Liverpool hadi kufikia sasa haijui ni lini nyota wao Mohamed Salah atarejea uwanjani kuendelea kuitumikia timu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Staa huyo mwenye umri wa miaka 27 aliumia kifundo cha mguu katika mechi dhidi ya Manchester City ambayo vinara hao walishinda kwa 3-1.

Mshambuliaji huyo alishindwa kumaliza mchezo huo na ilibidi aondolewe uwanjani katika kipindi cha pili kutokana na jeraha hilo ambalo lilimfanya akose mechi mbili za kufuzu kwa AFCON dhidi ya Harambee Stars ya Kenya na timu ya Visiwa vya Comoros.

Kukosekana kwa nyota huyo kikosini pamoja na wachezaji wengine muhimu kulivuruga juhudi za Misri ambayo ilitoka sare 1-1 na 0-0 dhidi ya Comoros.

Salah, anaendelea kupata matibabu katika klabu yake jijini hapa, lakini daktari hajatoa ripoti yoyote kuhusu hali yake.

Staa huyo amefunga mabao tisa katika mechi 17 msimu huu akiwa chini ya kocha Jurgen Klopp ambaye hadi sasa kikosi chake kinaongoza msimamo wa EPL.

Ingawa ameanza kufanya mazoezi mepesi, huenda nyota huyo pamoja na Andrew Robertson wasicheze mwishoni mwa wiki dhidi ya Crystal Palace.

Wote wamerejea mazoezini lakini hawajapata nafuu kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezewa Selhusrt Park, Jumamosi.

Dhidi ya Manchester City, Robertson alicheza dakika zote 90, huku Salah akitolewa mechi ikielekea kumalizika.

Iwapo wataikosa mechi hiyo, huenda wakawa kikosini Jumatano dhidi ya Napoli katika pambano la Ligi ya Klabu Bingwa litakalochezewa Anfield.

Lakini kocha Klopp atamkaribisha Joe Gomez ambaye alijiondoa katika kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza, pia kutokana na jeraha la goti.

Beki huyo tayari ameonyesha dalili za kuwa katika hali nzuri ya kucheza kuanzia wikendi hii, na huenda akapewa jukumu la kujaza nafasi ya Joel Matip anayeendelea kuuguza jeraha la goti.

Viungo Jordan Henderson na Georginho Wijnaldum wamekuwa wakitatizwa na majeraha, lakini huenda wakarejea Jumamosi.

Xherdan Shaqri

Xherdan Shaqri pia anatarajiwa kuwa fiti kucheza dhidi ya Crystal Palace, ingawa raia huyo wa Uswisi hajaanza mechi yoyote msimu huu.

Wakati huo huo, kocha Graeme Souness amebashiri kwamba mbio za Liverpool kwenye vita vya kuwania taji la EPL zinakaribia kuanza kupunguka.

Kocha huyo ambaye zamani aliichezea klabu hiyo ya Liverpool anaamini kwamba timu zilizo nyuma ya mabingwa hao wa Ulaya, ikiwemo Manchester City zitaanza kuifukuza kwa karibu na presha mbayo itaipa wasiwasi.

Alisema hata kama wataibuka mabingwa msimu huu, timu za Chelsea, Manchester United na Manchester City zitaanza kung’ara na kutawala misimu ujayo.

“Licha ya kikosi kuwa na vijana wengi, Chelsea itaibukia kuwa timu hatari katika misimu michache ijayo,” aliongeza.