Michezo

ITABIDI MZOEE: Wakala afichua Ozil haondoki Arsenal hivi karibuni

May 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

MESUT Ozil, 32, amezima tetesi zilizokuwa zikimhusisha na uwezekano wa kubanduka Arsenal kwa kufichua kwamba atasalia ugani Emirates kwa muhula mwingine mmoja kabla ya kuondoka rasmi mwishoni mwa msimu ujao.

Haya ni kwa mujibu wa wakala wake Erkut Sogut ambaye ameshikilia kwamba mteja wake huyo hana mipango yoyote ya kuagana na Arsenal hivi karibuni.

Awali, Ozil alikuwa akitarajiwa kujiunga na Fenerbahce ya Uturuki mwishoni mwa msimu huu baada ya Acun Ilicali ambaye ni rafikiye mkubwa na mtangazaji wa Turkish TV kutangaza kuwa Ozil amemweleza awaandae kisaikolojia mashabiki wa Ligi Kuu ya Uturuki kwamba atakuwa akinogesha kipute hicho msimu ujao.

“Nimekuwa nikipokea maswali mengi kuhusu Ozil. Naamini kwamba mambo mazuri yatamtendekea hivi karibuni. Atabanduka Arsenal mwishoni mwa msimu huu na atakuwa akivalia jezi za Fenerbahce muhula ujao,” akasema Ilicali katika mahojiano yake na kituo cha Sport Witness, Uturuki.

“Siwezi kufichua mengi zaidi ya haya ila ninafahamu kwamba Rais wa Uturuki anajitahidi sana kuona Ozil akiingia Fenerbahce haraka iwezekanavyo. Sidhani akisalia kusubiri zaidi mkataba wake na Arsenal utamatike kabla aje kutia ladha soka ya Uturuki,” akaongeza.

Kwa upande wake, Sogut ambaye ameelekea kuunga mkono kauli ya Ilicali, amesema kwamba mteja wake atakuwa radhi zaidi kubanduka Emirates muhula ujao bila ada yoyote na kituo chake cha kwanza kitakuwa Uturuki.

“Ozil angali na mwaka mmoja zaidi katika mkataba wake na Arsenal. Sidhani patatokea mabadiliko yoyote kuhusiana na hilo. Kitakachofanyika ni kwamba atakamilisha kipindi kizima cha kuhudumu kwake ugani Emirates kabla ya kutathmini ofa nyingine. Hata hivyo, tamanio lake ni kustaafu akisakata soka ya kulipwa nchini Uturuki,” akaongeza Sogut.

Kufikia sasa, Ozil hupokezwa mshahara wa hadi Sh49 milioni kwa wiki, fedha ambazo Arsenal watalazimika kumlipa kwa kipindi cha miezi mingine 12 ijayo.

Hili ni jambo ambalo kocha Mikel Arteta amedokeza kwamba litamzuia sana kujinasia huduma za baadhi ya wachezaji ambao amekuwa akitamani sana kusajili tangu apokezwe mikoba ya The Gunners mwishoni mwa mwaka wa 2019.