Jagina wa soka raia wa Senegal, Papa Bouba Diop aaga dunia
Na MASHIRIKA
NYOTA wa zamani wa Fulham, Portsmouth na timu ya taifa ya Senegal, Papa Bouba Diop aliaga dunia mnamo Novemba 29, 2020 akiwa na umri wa miaka 42.
Diop aliyewahi kuchezea pia West Ham United na Birmingham City, aliwajibishwa mara 129 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Alikuwa sehemu ya kikosi kilichotegemewa na Senegal katika fainali ya Kombe la Dunia mnamo 2002 na akafunga bao la pekee katika ushindi wa 1-0 uliosajiliwa na Senegal katika mchuano wa ufunguzi wa kivumbi hicho dhidi ya mabingwa watetezi Ufaransa.
“Diop alikuwa shujaa wa Kombe la Dunia. Hivyo ndivyo tunavyomjua,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwenye mtandao wao wa kijamii.
Kwa upande wao, Fulham walitumia mtandao wao wa Twitter kumwomboleza Diop. Usimamizi wa kikosi hicho ulisema: “Ni masikitiko makubwa kumpoteza Diop ambaye hapa kikosini tulimfahamu kama ‘Wardrobe’.
Ushawishi wa Diop uwanjani uliwasaidia Senegal kutinga hatua ya robo-fainali za Kombe la Dunia mnamo 2002 huku Diop akifunga mabao mawili zaidi katika sare ya 3-3 iliyosajiliwa na kikosi chake dhidi ya Uruguay kwenye hatua ya makundi.
Kabla ya kustaafu soka mnamo 2013, Diop alikuwa amenogesha fainali nne za Kombe la Afrika (AFCON) na alikuwa sehemu muhimu katika kikosi cha Senegal kilichoambulia nafasi ya pili kwenye kipute hicho mnamo 2002.
Diop alichochea pia Portsmouth kunyanyua ubingwa wa Kombe la FA mnamo 2008 chini ya mkufunzi Harry Redknapp.
“Kufa kwa Diop ni pigo kubwa kwa Senegal, makuzi na maendeleo ya soka ya taifa hilo,” akasema fowadi wa Liverpool Sadio Mane katika kauli iliyoshadidiwa na Rais wa Senegal, Macky Sall.