Jose Mourinho awakasirisha Man-United
Na MASHIRIKA
LONDON, Uingereza
KOCHA Jose Mourinho amesema timu yake ya zamani, Manchester United haitamaliza miongoni mwa nne-bora katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), msimu huu.
Alipoulizwa afafanue zaidi, Mourinho alisema kuwa mbali na Liverpool, timu zingine katika mduara huo zitakuwa Manchester City, Leicester City na Chelsea au Tottenham Hotspur.
Hata hivyo, kocha huyo Mreno alisema Everton, Man-United na Wolves zina nafasi finyu akiongeza kwamba haoni dalili za Arsenal kukaribia orodha hiyo.
“Wolves na Sheffield United zinazidi kushangaza, wakufunzi wao hawatakubaliana nami lakini ukweli ndio huo.
“Nafasi walimo kwa sasa haziwezi kuthibitisha ninayosema, lakini hivyo ndivyo ninavyoona,” Mourinho aliwaambia waandishi.
“Wamo katika nafasi hizo kinyume na matarajio ya wengi, na kwa hakika wanapaswa kufurahia hatua hiyo.
“Wolves walisajili mchezaji muhimu Daniel Podence kwa lengo la kuimarisha kikosi chao. Sheffield ilifanikiwa kumtwaa Sander Berge, na usajili huo umewasaidia kwa kiasi kikubwa.”
Kuhusu klabu yake ya Tottenham, Mourinho alisema ushindi wao wa majuzi wa 2-0 dhidi ya Man-City umewaongezea matumaini ya kumaliza miongoni mwa 4-bora, hasa ikikumbukwa kwamba Chelsea watakuwa ugenini kucheza na Man-United hapo Februari 17.
Katika habari zinginezo, mshambuliaji matata Emmanuel Adebayor, 35, raia wa Togo amesajiliwa na Club Olimpia ya Paraguay.
Mbali na nchini Paraguay, Adebayor aliwahi kuchezea klabu maarufu nchini Ufaransa, Uingereza, Uhispania na Uturuki.
Ujio wa Adebayor umewapa matumaini makubwa mashabiki wa Club Olimpia, ambayo pia inajivunia aliyekuwa mshambuliaji matata wa Bayern Munich, Roque Santa Cruz aliye nahodha wao.
Wakati wake, Adebayor alizichezea klabu za Metz kati ya 2001 na2003, Monaco 2003-2006, Arsenal 2006-2009, Man-City 2009-2012, Real Madrid kwa mkopo 2011, Tottenham kwa mkopo 2011-2012 na kisha kwa mkataba wa kudumu 2012-2015, Crystal Palace 2016, Istanbul Basaksehir 2017-2019, na Kayserispor 2019 kabla ya kujiunga na Club Olimpia kwa sasa.