KCB yatuza kikosi cha voliboli
Na CHRIS ADUNGO
JITIHADA za wanavoliboli wa kikosi cha KCB zilitambuliwa Jumanne na Benki ya Kenya Commercial iliyowatuza jumla ya Sh150,000 kutokana na mafanikio yao ya majuma mawili yaliyopita mjini Bungoma.
Katika kampeni hizo, KCB iliwakomoa KDF katika mchuano wa ufunguzi wa msimu huu kwenye kipute cha KVF kabla ya kuwapokeza DCI kichapo cha 3-1.
Kwa mujibu wa Judith Sidi Odhiambo ambaye ni mlezi wa kikosi hicho, Benki ya KCB imepania kuwapiga jeki magwiji hao wa voliboli ya humu nchini kadri wanavyojitahidi kujifua upya kwa matumaini ya kutia kapuni ufalme wa Klabu Bingwa barani Afrika mwaka huu.
“Ni tija na fahari tele kwamba matokeo bora yanayozidi kusajiliwa na kikosi cha KCB msimu huu yatakuwa kiini cha hamasa ya klabu hiyo ambayo kwa sasa imejipa malengo ya kuvuna ushindi katika mingi ya michuano iliyosalia msimu huu,” akasema Sidi katika hafla hiyo ya jana iliyohudhuriwa pia na majagina wa zamani wa kikosi cha voliboli cha KCB –
Njeri Onyango, Rose Wanjala, Ann Wahombe na Dorcas Tidi.
Wachezaji hao wa zamani wa KCB waliwataka vipusa ambao kwa sasa wanaunga na kukamilisha kikosi hicho kuwaiga baadhi yao na kujitahidi vilivyo kila wanapopeperusha bendera ya klabu katika michuano ya kitaifa na kimataifa.
Katika juhudi za kudumisha uhai wa matumaini yao katika kampeni za voliboli msimu huu, KCB ilisuka upya timu ya wanawake kwa kujinasia huduma za wachezaji wanane. Kwa mujibu wa kocha mkuu wa KCB, Vernon Khayinga, usajili wa wachezaji hao ni hatua ya kimakusudi inayolenga kuzidisha viwango vya ushindani na kuiongezea timu hiyo uthabiti ambao utaiwezesha kuhimili mawimbi ya ushindani kutoka kwa wapinzani wakuu katika kampeni za KVF na za kimataifa.
Nyota hao ni pamoja na kiungo Caroline Sirengo, 21, ambaye aliagana rasmi na Kenya Prison na Lincy Jeruto aliyetokea Nairobi Water baada ya miaka miwili.
Lincy atashirikiana na Millicent Wanjala aliyebanduka kambini mwa wasomi wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU). Wengine ambao uzoefu wao unatazamiwa kuwavunia KCB nafuu kubwa ni mvamizi wa zamani wa Kwanthanze, Lucy Mumo, Metrin Wabwile aliyetokea Bungoma Bombers, Egline Kulova, Nancy Mulonza na Peris Kanus wa Kosirai Girls.