Michezo

Kenya Simbas wapigwa jeki na KQ kwa Sh15 milioni kabla ya kupepeta UAE

Na GEOFFREY ANENE May 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WANARAGA wa Kenya Simbas wamepata motisha kubwa kabla ya Kombe la Afrika 2025 la kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2027 baada ya Kenya Airways kuwapiga jeki ya Sh15 milioni Jumamosi, Mei 24, 2025.

Ushirikiano kati ya Shirikisho la Raga Kenya (KRU) na shirika hilo la ndege ulitangazwa saa chache kabla ya Simbas kubomoa Milki za Kiarabu 54-24 katika mechi ya kimataifa ugani RFUEA mjini Nairobi.

Udhamini huo utakuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha mipango ya Simbas kusafiri.

Vijana wa kocha Jerome Paarwater wameratibiwa kusafiri Mei 28 kuelekea kambi ya mazoezi ya wiki tatu nchini Afrika Kusini, kabla ya kurejea nyumbani na kisha kusafiri hadi mjini Kampala hapo Julai 3 kwa mechi ya ufunguzi dhidi ya wenyeji Uganda katika robo-fainali.

Afisa Mkuu Mtendaji wa KRU, Thomas Odundo, alizungumza wakati wa uzinduzi na kushukuru Kenya Airways. “Asanteni sana kwa niaba ya KRU,” alisema, akitambua mchango muhimu ambao shirika hilo litatoa katika kusaidia dhamira ya Simbas.

Mwenyekiti wa KRU, Alexander ‘Sasha’ Mutai, alielezea umuhimu wa kimkakati wa ushirikiano huo, akisema: “KQ wamekuwa nasi awali na tunafurahi kuwa nao tena. Huu ni udhamini muhimu sana kwani kuwa na shirika la ndege kama mshirika kunapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za usafiri. Simbas wanapoanza safari yao ya kufuzu Kombe la Dunia, hii ni hatua kubwa nzuri. Tunashukuru sana na tunatumai ushirikiano huu utaingia katika timu nyingine kama Under-20, Shujaa, na Lionesses.”

Afisa Mkuu wa Kibiashara na Huduma kwa Wateja wa Kenya Airways, Julius Thairu, alithibitisha tena kujitolea kwa shirika hilo. “Tumerejea kwenye raga. Kwa niaba ya Afisa Mtendaji wetu, tunafurahi na kujivunia kuwa sehemu ya safari ya Simbas wanapolenga nafasi katika Kombe la Dunia. Hatuangalii tu udhamini, bali pia maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Kuna vipaji vingi nchini Kenya, na kama chapa, tungependa kusaidia kukuza na kuviangazia. Tutaandamana katika safari hii pamoja. Huu ni mwanzo tu, na pia tunatazamia kusaidia timu nyingine za taifa,” akasema.

Nahodha wa Simbas, George Nyambua, alizungumza kwa niaba ya timu na kuonyesha shukrani ya dhati kwa udhamini huo. “Tunasema asante sana. Udhamini huu utakuwa na athari kubwa katika safari yetu ya kufuzu. Tunaamini tutafuzu na kuwafanya mjivunie.”

Kupitia usaidizi huo mpya, Simbas sasa wanaelekeza macho yao katika kuandika historia kwani hawajawahi kuingia Kombe la Dunia tangu waanze kujaribu kutafuta tiketi mwaka 1995.