Michezo

Kenya U-17 yatinga nusu fainali licha ya kupigwa 1-0 na Somalia

April 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imeingia nusu-fainali ya mashindano ya soka ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17 ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) yanayopamba moto nchini Burundi licha ya kuendelea kuandikisha matokeo mabaya.

Baada ya kupepeta Burundi 4-0 katika mechi ya ufunguzi ya Kundi A na kukabwa 0-0 na Ethiopia katika mechi ya pili, vijana wa kocha Michael Amenga walinyukwa 1-0 na Somalia katika mechi yao ya mwisho ya makundi Ijumaa.

Dhidi ya Burundi, Kenya ilivuna ushindi kupitia mabao ya Isaiah Abwal (mawili), Christopher Raila na Nicholas Omondi mnamo Aprili 14.

Mabao ‘yalikauka’ katika sare tasa dhidi ya Ethiopia hapo Aprili 17 kabla ya mambo kuharibika hata zaidi ilipozamishwa 1-0 na Somalia kupitia bao la Farhan Mohamed Ahmed lililopatikana dakika ya 15.

Kenya ilijkatia tiketi kwa kumaliza mechi za makundi ya pili kwa alama nne. Somalia ilikamilisha juu ya jedwali kwa alama saba. Ilipewa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ethiopia katika mechi ya ufunguzi baada ya Ethiopia kupatikana imechezesha wachezaji watatu waliopitisha umri wa miaka 17.

Ilitoka sare tasa dhidi ya Burundi katika mechi ya pili kabla ya kukumbusha Kenya taji halikuja kwa urahisi kwa kuipiga 1-0. Ilitumia mfumo wa kucheza wa mabeki watano, viungo wanne na mshambuliaji mmoja (5-4-1) kuangamiza Kenya.

Burundi ilikamilisha mechi zake za makundi kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Ethiopia, lakini matokeo haya hayakusaidia mataifa haya mawili kusalia mashindanoni.

Katika mechi za Kundi B, Uganda ilibwaga Sudan 3-0 na kuingia nusu-fainali kwa jumla ya alama nne baada ya kukaba Tanzania 1-1 katika mechi ya ufunguzi. Timu ya mwisho kufuzu kushiriki nusu-fainali itafahamika Jumapili pale Tanzania na Sudan zitakapoteremka uwanjani kumaliza udhia.

Kundi hili lilibaki na timu tatu baada ya Zanzibar kutimuliwa kwa kuwasili nchini Burundi na wachezaji 12 waliozidi umri wa miaka 17 katika kikosi chake.

Ethiopia na Zanzibar zilipigwa faini ya Sh500,252 na Sh1,500,757, mtawalia.