Kenya yapangwa na Burundi katika mchujo wa CHAN
KENYA watakuwa wenyeji wa Burundi kati ya Julai 26-28 katika mkondo wa kwanza wa mchuano wa kufuzu kwa fainali za CHAN 2020.
Itakuwa mara ya kwanza kwa Kenya kuwania ubingwa wa CHAN baada ya kupokonywa fursa ya uenyeji wa fainali hizo zilizoandaliwa baadaye na Morocco kutokana na maandalizi duni.
Harambee Stars watashuka dimbani kwa minajili ya marudiano dhidi ya Burundi kati ya Agosti 2-4 jijini Bujumbura.
Mshindi wa mechi hizo za mikondo miwili atajikatia tiketi ya kuvaana na ama Tanzania au Sudan katika raundi ya pili na ya mwisho itakayoshuhudia mkondo wa kwanza ukipigwa kati ya Septemba 20-22 huku marudiano yakiandaliwa kati ya Oktoba 18-20.
Kikosi kitakachoibuka mshindi wa raundi ya mwisho atachuana na Ethiopia ambao watakuwa wenyeji wa fainali za CHAN zitakazowashirikisha wachezaji wa klabu za nyumbani pekee kuanzia Januari 2020.
Wakati uo huo, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) limethibitisha tarehe na uwanja wa kuchezewa mchuano wa mwisho wa Kundi F utakaokutanisha Ghana na Kenya katika safari ya kufuzu kwa Kombe la Afrika (AFCON) 2019.
Kwa mujibu wa CAF, kivumbi hicho kati ya timu hizo ambazo tayari zimefuzu kwa fainali za AFCON, kitatandazwa uwanjani Ohene Gyan Sports jijini Accra mnamo Machi 23.
Kujifua kwa fainali
Kutamatika kwa mechi hiyo kutatoa fursa kwa vikosi vyote viwili kujifua kwa fainali zitakazoandaliwa nchini Misri kati ya Juni 21 na Julai 19.
Itakuwa mara ya kwanza baada ya miaka 15 kwa Kenya kuwania ufalme wa AFCON baada ya kubanduliwa kwenye hatua ya makundi mnamo 2004 jijini Tunis, Tunisia.
Ushindi wa 3-1 dhidi ya Burkina Faso ndio wa pekee uliosajiliwa na Harambee Stars ya Kenya katika fainali hizo.
Kenya walifungua kampeni zao za makundi kwa kupoteza ugenini dhidi ya Sierra Leone ambao baadaye waliondolewa na CAF kwenye kivumbi cha mwaka 2019.
Ushindi dhidi ya Ghana jijini Nairobi kabla ya kujizolea alama nne muhimu dhidi ya Ethiopia katika michuano ya mikondo miwili nyumbani na ugenini; ni ufanisi uliowezesha Kenya kufuzu.
Chini ya mkufunzi Sebastien Migne ambaye ni mzawa wa Ufaransa, Kenya kwa sasa inadhibiti kilele cha Kundi F kwa alama saba, moja zaidi kuliko Ghana.
Ethiopia waliokuwa pia wakiunga kundi hili, walibanduliwa mapema.
Itakuwa mara ya kwanza kwa Ghana kuchezea jijini Accra tangu 2016 walipowadhalilisha Mauritius kwa mabao 7-1 katika mojawapo ya mechi za kufuzu kwa fainali za AFCON 2017.
Sare au ushindi kwa Ghana utawapaisha hadi kileleni mwa Kundi F na kusalia na matarajio ya kutiwa katika zizi jepesi droo ya fainali za AFCON 2019 itakapofanywa jijini Cairo, Misri mnamo Aprili 12.
Japo Rais Nick Mwendwa wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) amewapa Stars malengo ya kutinga robo-fainali za kipute cha AFCON, wachanganuzi wa soka wanahisi kwamba huenda ikamwia vigumu kocha Migne kuyafikia maazimio hayo.
Kulingana na kocha wa zamani wa Stars, Bandari na KCB Rishad Shedu, Kenya haina miungo-mbinu maridhawa za kuwakuza chipukizi wanaojivunia utajiri mkubwa wa vipaji na talanta za kupiga soka.
Kulingana naye, mengi ya mataifa ambayo tayari yamefuzu kwa fainali hizo yamewekeza sana katika miradi ya kuchangia makuzi ya wanasoka chipukizi ambao watakuwa tegemeo la takriban kila kikosi nchini Misri.
Mbali na kumtaka Migne kusuka kikosi chake kwa mseto wa wachezaji wazoefu na chipukizi, Shedu ameeleza pia haja ya kukishirikisha kikosi cha Stars kwa miechi nyingi za kujipima nguvu ili kuchangia uthabiti zaidi wa kila idara.
Hofu zaidi ni kwamba huenda wachezaji wa Ligi Kuu ya KPL watakaotegemewa na Migne kwenye AFCON wakalemewa na uchovu na mavune iwapo wataendelea kuwajibishwa kwa zaidi ya mara tatu kwa wiki kama ilivyo kwa sasa ligini.