• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
KITANUKA! Ni gozi la mashemeji fainali ya UEFA

KITANUKA! Ni gozi la mashemeji fainali ya UEFA

Na MASHIRIKA

NAIROBI, Kenya

LIVERPOOL na Tottenham Hotspur zitaumiza nyasi uwanjani Wanda Metropolitano nchini Uhispania Jumamosi usiku katika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya ambayo Wakenya wameibandika ‘gozi la Mashemeji’ kutokana na kuwakutanisha Divock Origi na Victor Wanyama.

Mbelgiji mwenye asili ya Kenya Origi anachezea Liverpool, ambayo pia itawategemea sana Sadio Mane, Mohamed Salah na Jordan Henderson. Mabingwa hawa wa Bara Ulaya mwaka 1977, 1978, 1981, 1984 na 2005 watakuwa wakitafuta kumaliza ukame wa miaka minane bila taji.

Nahodha wa Harambee Stars Wanyama ni mchezaji wa Tottenham ambayo inajivunia wakali kama Son Heung-min na Lucas Moura.

Spurs ina ukame hata zaidi wa mataji ambapo imewahi kushinda mashindano ya daraja la pili ya Bara Ulaya mwaka 1963, 1972 na 1984.

Taji la mwisho la Liverpool na Spurs ni katika League Cup nchini Uingereza mwaka 2012 na 2008 mtawalia.

Wachezaji Harry Kane (Tottenham) na Roberto Firmino (Liverpool) wanatarajiwa kuwa fiti kushiriki mchuano huu baada ya kusumbuliwa na jeraha la kifundo na kinena katika mwezi wa mwisho wa Ligi Kuu.

Huenda hali yao ya kujumuishwa kikosini ikajulikana mapema Jumamosi.

Nchini Kenya, taifa la watu 50 milioni, ambalo linaenzi soka, litakuwa likifuatilia fainali hii kwa karibu sana likitumai Origi na Wanyama wataliweka kwenye ramani ya dunia kwa mchango muhimu.

Huku Wakenya wakisubiri kwa hamu kubwa Kombe la Bara Afrika (AFCON) mwezi Juni/Julai, fainali ya Klabu Bingwa imewagawanya.

Katika klabu ya Ligi Ndogo jijini Nairobi, kocha Kenneth Amolo alijitapa akisema, “Hii ni mara ya kwanza wachezaji walio na asili ya Kenya wanashiriki katika fainali ya Klabu Bingwa. Kiungo Wanyama na mshambuliaji Origi watawakilisha Kenya katika ulingo wa dunia, inafurahisha sana.”

Naye kocha Lawrence Omondi aliambia shirika la habari la AFP kwamba atakuwa akishabikia Spurs kwa sababu “Wanyama ni nahodha wa timu ya taifa ya Kenya, na mchezaji wetu bora anayestahili kuungwa mkono.”

Bao

Wanyama si kiungo shupavu tu, bali pia ni Mkenya wa kwanza kufunga bao katika mchuano wa Klabu Bingwa Ulaya alipoongoza Celtic kulima Barcelona 2-1 mwaka 2012.

Wanyama alianza mechi 13 pekee katika ligi ya Uingereza msimu huu, lakini amesakatia Spurs mara sita katika michuano ya Klabu Bingwa na anashabikiwa na wapenzi wa soka katika klabu hiyo.

Origi, kwa upande wake, amekuwa na mchango mkubwa katika Klabu Bingwa alipopachika mabao mawili uwanjani Anfield na kusaidia Liverpool kubandua Barcelona katika nusu-fainali.

Ingawa Origi, ambaye alijiunga na Liverpool akitokea Lille nchini Ufaransa, huchezea Ubelgiji, pia anapendwa na mashabiki wa soka nchini Kenya, hasa kutokana na kwamba babaye Mike Okoth alikuwa nahodha wa Stars.

“Divock alizaliwa na kulelewa Ubelgiji, lakini bado ana uhusiano na Kenya,” alisema mjombake Austin Oduor, ambaye pia aling’ara akiwakilisha Kenya.

“Yeye huja Kenya mara kwa mara na anazungumza Kiswahili,” aliongeza.

Wachezaji hawa wawili watawakilisha jamii mbili nchini zenye uhasama mkubwa kisoka.

“Origi anatoka katika jamii ya Waluo, naye Wanyama ni Mluhya,” anasema mwandishi wa habari za michezo Elias Makori. Jamii hizi mbili zimehusishwa na soka ya Kenya kwa muda mrefu, huku Waluo na Waluhya wakishabikia Gor Mahia na AFC Leopards, mtawalia.

Hii ndiyo sababu mechi hii imepata jina jipya “Mashemeji derby”, Wakenya wakirejelea gozi kati ya klabu hizi.

You can share this post!

MWANAMKE MWELEDI: Licha ya dhoruba kali, hakutikisika

Mwilu aponyoka kesi ya ufisadi, DPP aahidi rufaa

adminleo