Kocha wa Western Stima asema Omala yuko huru kuhamia timu nyingine
Na CECIL ODONGO
KOCHA wa Western Stima Salim Babu amesema hatamzuia mshambuliaji nyota wa klabu hiyo Benson Omala kuhama huku mwanasoka huyo akiripotiwa kuwa anaviziwa na timu za haiba zinazoshiriki Ligi Kuu Nchini (KPL).
Babu alisema Omala mwenye umri wa miaka 17 pekee amedhihirisha kwamba huenda akawa mwanadimba nguli siku zijazo na hawezi kumkwamilia iwapo anapata ujira mzuri kwingine.
Mwanafunzi huyo wa kidato cha nne katika Shule ya Upili ya Kisumu Day amekuwa mhimili mkubwa kwenye kikosi cha wanaumeme hao na alishawatingia mabao manane kabla ya mechi za KPL kusitishwa kwa muda kutokana na janga la virusi vya corona.
“Mimi huwatakia wachezaji wangu mema na huhisi vyema kazi wanayoifanya uwanjani ikitambuliwa na wao kumiminiwa sifa kedekede. Nimesikia kwamba Omala yupo njiani kuondoka na huenda hatutakuwa naye msimu ujao.
“Iwapo itatokea hivyo kwenye dirisha dogo la uhamisho wa wachezaji, basi sitamzuia ila kumtakia mema. Yeye ni mchezaji chipukizi ambaye atang’aa zaidi akimakinikie taaluma yake,” akasema Babu kwenye mahojiano na Taifa Leo.
Hata hivyo, Babu alikataa kufichua timu ambazo zinawania huduma za Omala kama mpira wa kona, akisema zitajulikana wakati wa uhamisho wa wachezaji.
“Kumekuwa na taarifa kotekote kwamba atahamia timu nyingine. Binafsi nimemuuliza kama kuna timu ambayo imemfikia kibinafsi lakini hakunifichulia. Kwa kuwa ni mtahiniwa, kwa sasa anamakinikia masomo yake ili apitie mtihani wake wa KCSE,” akaongeza Babu.
Duru hata hivyo zinaarifu kwamba Gor Mahia wapo mstari wa mbele kumsajili mshambulizi huyo ili kuimarisha safu yao ya ushambizi ambayo imesenea sana msimu huu.
Kabla ya kujiunga na Stima, Omala alikuwa akisakatia Manyatta FC ya Kisumu inayoshiriki Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka Nchini (FKF) divisheni ya pili.
Mvamizi huyo mahiri alijiweka kwenye kumbukumbu za kihistoria kwa kuwa mchezaji mdogo zaidi nchini kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa KPL.
Aliibuka mwanadimba bora wa ligi mwezi Desemba na aliikabidhiwa tunu hiyo Januari mwaka huu kwenye hafla ya kipekee mjini Kisumu.
Kando na kuwa kwenye kikosi cha kwanza cha Western Stima, Omala alikuwa mchezaji wa kwanza wa timu hiyo kufunga ‘hat-trick’ kwenye mechi ya ligi, pale wanaumeme hao waliwazidi marina Zoo Kericho kwa kuwachabanga 4-1 mnamo Desemba.
Western Stima inashikilia nafasi ya saba kwenye msimamo wa jedwali la KPL kwa alama 36 baada ya kujibwaga uwanjani mara 23.
Mwenyekiti wa klabu hiyo Laban Jobita naye amenukuliwa akiunga mkono hatua ya Mwenyekiti wa FKF Nick Mwendwa ya kutangaza Gor Mahia mabingwa wa KPL na kutamatisha ligi zikiwa zimesalia mechi 10 zimalizike.