Michezo

La Liga ilivyopoteza ladha bila ya Neymar, Ronaldo kwa mkupuo

December 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

Rais wa Barcelona Josep Bartomeu majuzi alisema kwamba kubanduka kwa nyota Cristiano Ronaldo na Neymar katika soka ya Uhispania kumeshusha sana viwango vya ushindani katika Ligi Kuu ya La Liga.

Isitoshe, aliungama kuwa matokeo ya wawili hao kuon- doka nchini Uhispania ni kushuka kwa sasa kwa umaarufu wa La Liga, kivumbi ambacho kwa mujibu wa Bartomeu, kinastahili kuwa katika kiwango sawa na Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Neymar ambaye ni mvamizi matata mzawa wa Brazil, aliagana rasmi na Barcelona mwishoni mwa msimu wa 2016-17 na kutua jijini Paris, Ufaransa kuvalia jezi za Paris Saint-Germain (PSG) ambao kwa kipindi kirefu, wameku- wa wakitamalaki na kutawala soka ya Ligi Kuu ya Ligue 1.

Kwa upande wake, Ronaldo alikatiza ghafla uhusiano wake na Real Madrid ambao ni mabingwa watetezi wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na kuhiari kuelekea Italia kuwasakatia miamba wa Ligi Kuu ya Serie A, Juventus. Kulingana na Bartomeu, uwepo wa Ronaldo kambini mwa Juventus ni jambo linaloweka kikosi hicho katika uwezekano mkubwa wa kutawazwa mabingwa wa UEFA msimu huu.

Kufikia sasa, Juventus wanaselelea kileleni mwa Kundi H kwa alama 12, mbili Zaidi kuliko Manchester United ambao wanatarajiwa pia kutinga hatua ya mwondoano.

Young Boys wanaburuza mkia kwenye kundi hilo linalowajumuisha pia Valencia ambao kwa sasa wanatazamiwa kuteremka ngazi kuwania ubingwa wa Ligi ya Uropa.

“Inasikitisha kwamba La Liga kwa sasa imepoteza wachezaji wawili wa haiba kubwa baada ya kipindi cha miaka miwili pekee,” akatanguliza Bartomeu.

“Kuondoka kwa Ronaldo ni pigo kubwa zaidi kwa soka ya Uhispania. Hatua hiyo italemaza hata zaidi viwango vya ushindani katika La Liga, na hivyo kudidimiza makali ya Real ambao siku zote wameongozwa na dhamira ya kutandaza soka safi ya kuvutia ili kufikia viwango vya Barcelona,” akasema kinara huyo.

Kwa mujibu wa Bartomeu, ushindani mkali ambao umekuwa ukitawala soka inayopigwa na Real na Barcelona ni kiini cha Ligi ya Uhispania kujivunia idadi kubwa ya mashabiki duniani sawa na hali ilivyo katika EPL.

Ingawa hivyo, kinara huyo anashikilia kuwa kikubwa zaidi kinachofanya EPL kwa nyakati fulani kuwa na umaarufu zaidi kuliko La Liga ni wingi wa fedha ambazo humwagwa sokoni na wamiliki, wala si ubora wa soka inayopigwa viwanjani.

“Kudumisha masogora wa haiba kubwa ligini ndiyo siri ya pekee ya kuendeleza viwango vya ushindani kati ya La Liga na EPL – vipute viwili ambavyo ni maarufu zaidi kati ya Ligi Kuu tano mashuhuri za bara Ulaya, yaani Serie A (Italia), Bunde- sliga (Ujerumani) na Ligue 1 (Ufaransa). Ronaldo hachangii tu uthabiti wa Juventus. Pia anaboresha kampeni nzima za Serie A na kuwaweka waajiri wake katika nafasi nzuri zaidi ya kunyanyua ufalme wa UEFA msimu huu,” akasema Bartomeu katika kauli iliyowiana na ya nahodha wa Barcelona, Lionel Messi.

Kulingana na Messi, ushawishi wa Ronaldo uwanjani ni miongoni mwa mambo yanayowaweka Juventus katika kundi moja na wagombeaji halisi wa taji la UEFA muhula huu.

Japo Barcelona wanadhibiti kilele cha La Liga, pengo la alama kati yao na wapinzani wao wakuu wanaofunga mduara wa tano-bora ni dogo sana.

Kusuasua kwa miamba hao ni jambo ambalo Bartomeu amehusisha na kuondoka kwa Ronaldo ambaye alikuwa kiini cha kuimarika kila uchao kwa makali ya Messi na Barcelona ambao pia wanatazamiwa kusonga mbele katika UEFA.