Liverpool kuvaana na Man City kwenye robo fainali UEFA
Na CECIL ODONGO
KIPUTE cha kuwania ubingwa wa soka Bara Uropa kinatarajiwa kunogeshwa zaidi baada ya ratiba inayoshirikisha timu nane mibabe zitakazochuana kwenye robo fainali kutolewa Ijumaa.
Mashabiki wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) yenye mashabiki wengi zaidi duniani watakuwa na fursa nyingine ya kutazama pambano kubwa kati ya klabu za Liverpool na Man City kwenye anga za soka ya Bara. Kufikia sasa klabu hizi mbili zimeongoza kwa ufungaji wa magoli ligini EPL.
Liverpool ambao wanarekodi nzuri ya kutia kibindoni kombe hilo mara tano, iliwapa Mancity wanoelekea kutwaa ubingwa wa EPL mabao 4-3 kwenye mchuano wa ligi mwezi Januari uwanjani Anfield. Hii ni baada ya vijana hao wa kocha Pep Guardiola kuiadhibu Liverpool 5-0 ugani Etihad.
Klabu hizi zinajivunia mastaa washambuliaji Sergio Aguero, Gabriel Jesus na Leroy Sane kwa upande wa Man City, na Mohammed Salah, Sadio Mane na Roberto Firmino kwa upande wa The Reds.
Ratiba hiyo itashuhudia mabingwa watetezi Real Madrid wakivaana na mabingwa wa Serie A Juventus, Barcelona ya Uhispania watifue kivumbi dhidi ya Roma ya Italia na Sevilla wapambane na wafalme wa Ujerumani, Bayern Munich.
Kulingana uchanganuzi wa kina na historia ya kipute hiki, mchuano kati ya Juventus na Madrid ambao walishiriki fainali ya mwaka 2017 utanatazamiwa kuzua msisimko.
Juve watapigana kwa jino na ukucha kulipiza kisasi cha kupoteza fainali ya mwaka 2017 kando na kwamba kipa wao mkongwe Gianliugi Buffon aliye na umri wa miaka 40 atakuwa anastaafu.
Japo ana historia pevu kwenye fani ya soka, Buffon hajawahi kushinda kombe hili la hadhi ya juu kwenye ulimwengu wa soka.
Real Madrid kwa upande wao watakuwa wanaazimia kuandikisha historia mpya kwa kushinda kombe hilo kwa mara ya tatu kwa mpigo.
Mechi kati ya Barcelona na Roma na Sevilla dhidi ya Bayern Munich pia zinatarajiwa kuwa kali.
Michuano ya mkondo wa kwanza itasakatwa tarehe 3 na 4 mwezi Mei huku wa pili ukichezwa tarehe 10 na 11 mwezi uo huo.