Michezo

Mashabiki wamlia Rachier Gor ikining'inia pabaya CAF

April 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

MASHABIKI wa Gor Mahia, wanaofahamika kwa jina la utani kama The Green Army, wameelekeza bunduki zao kwa viongozi wa klabu hiyo wakisema walichangia pakubwa mabingwa hao wa Kenya kulimwa 2-0 na Berkane ya Morocco katika mechi ya robo-fainali ya mkondo wa kwanza Jumapili.

Wamelaumu uongozi wa Ambrose Rachier kwa kutowajali wachezaji kwa kuchelewesha mishahara yao na kuwafanya kugoma mara kwa mara; jambo ambalo pia limeathiri vibaya motisha kikosini.

Wakizungumza baada ya kichapo hicho kikali kilichopatikana pale kiungo Francis Kahata alipojifunga na Bakr El Helali akagonga msumari wa mwisho, mashabiki wamesema matokeo mazuri hayapatikani viongozi wasipowapa wachezaji haki yao.

Shabiki Tillen Ndong’a alisema, “Kama bado viongozi wa Gor Mahia wataendelea kukera wachezaji kwa kuwalipa mishahara kuchelewa ama kutowalipa, basi hatutaenda mbali. Vijana wanastahili kuona matunda ya jasho lao baada ya kutuwakilisha vyema. Licha ya klabu kuvuna mamilioni kwa kufika robo-fainali na pia kuwa na mdhamini bilionea, wachezaji wetu bado hawapati mishahara, kiasi cha kuwafanya wasusie mazoezi, aibu ilioje! Viongozi mmetusikitisha sana!!!”

Naye Michael Njagi Ramadhani alisema, “Haya ndiyo matokeo ya kucheza na fedha za wachezaji… Viongozi wa Gor ni bure. Pia, nalaumu wadhamini SportPesa kwa kuwekeza fedha nyingi wakifahamu vyema kuna viongozi walio na “mikono gamu” inayokataa kulipa marupurupu eti kwa sababu mtu anapokea mshahara.”

Naye Loud Necessary Noise aliandika katika ukurasa wake wa Facebook, “Lipeni wachezaji jameni, mkiambiwa mnasema tunawasumbua, lakini malipo huwapa wachezaji motisha ya kucheza ….”

Kulipa

Inasemekana wachezaji wa Gor walipanga kususia mechi dhidi ya Berkane uwanjani Kasarani, hatua ambayo ilisukuma viongozi hao kuwalipa fedha zao.

Madhara hata hivyo, yalikuwa yameshafanyika kwani wachezaji hawakujitokeza mazoezini Jumamosi.

Gor, ambayo iko katika hatari ya kuwapoteza Kahata na mfumaji matata kutoka Rwanda Jacques Tuyisenge wanaosalia na chini ya miezi mitatu katika kandarasi zao, watalazimika kuchabanga Berkane 3-0 nchini Morocco ili kusonga mbele.

Mabingwa hawa wa Kenya mara 17, ambao wananolewa na Hassan Oktay, wana rekodi mbaya ya ugenini na inaonekana kama mambo kwisha.

Watamkaribisha beki Harun Shakava, lakini bado Tuyisenge, Shafik Batambuze na Ernest Wendo watakuwa akitumikia adhabu kutoka kwa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).