Michezo

Mbappe aomba mshindi wa Ballon d'Or awe Mfaransa

November 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

NA CECIL ODONGO

MWANASOKA chipukizi wa mibabe wa soka nchini Ufaransa PSG, Kylian Mbappe anaamini kwamba mchezaji bora ulimwenguni atakayeshinda tuzo za Ballon d’Or  Disemba 3, 2018 anafaa kutoka katika kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa kilichotwaa Kombe la Dunia nchini Urusi mwezi Julai, 2018.

Lionel Messi na Cristiano Ronaldo ambao  wameshinda tuzo hiyo mara tano kila moja pia wapo kwenye kiny’ang’anyiro hicho  ingawa wachanganuzi wengi wa soka wanaamini kwamba mwaka huu mchezaji mpya kando na wawili hao atashinda tuzo hiyo.

Nyota wa Chelsea raia wa Ubelgiji Eden Hazard na mshindi wa tuzo ya mwanasoka bora wa kiume wa Shirikisho la soka Duniani FIFA Luka Modric ni miongoni mwa walio katika hali nzuri kushinda tuzo hiyo.

Mbappe ambaye alitajwa kama mwanasoka bora chipukizi kwenye fainali za kombe la Dunia, 2018 nchini Urusi pia atakuwa akiwania kushinda japo amesema kwamba hata ikimponyoka itakuwa fahari kubwa iwapo mchezaji mwenza kutoka kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa, Les Blues ataishinda.

“Kuna wawaniaji wengi mwaka huu na kuna uwezekano wachezaji wengi wanaweza kuishinda. Natumai mshindi atakuwa mfaransa ili tuiongezee kombe letu la Dunia. Hata hivyo ushindani ni mkali na siwezi kutabiri mshindi,” akasema Mbappe.