MIA SAN MIA: Bayern wabomoa ukuta wa Union Berlin
CHRIS ADUNGO na MASHIRIKA
BAYERN Munich ambao ni viongozi wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) wamerejea katika kipute hicho kwa matao ya juu baada ya kuwachabanga Union Berlin 2-0 ugani Ander Alten Forsterei.
Robert Lewandowski aliwafungulia Bayern ukurasa wa mabao kupitia penalti kunako dakika ya 40 kabla ya Benjamin Pavard kukizamisha kabisa chombo cha wenyeji wao mwishoni mwa kipindi cha pili.
Bao la Lewandowski lilikuwa lake la 40 kutokana na mechi 34 ambazo amechezea Bayern katika michuano yote hadi kufikia sasa msimu huu. Goli la Pavard lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Joshua Kimmich.
Kivumbi cha La Liga kilianza upya mnamo Mei 16, 2020, huku wachezaji, wanahabari na maafisa wa afya, usalama na vikosi husika michuanoni wakizingatia kanuni mpya za afya.
Shughuli za wachezaji kupiga njaramba zilikosa ukawaida huku wachezaji wa akiba wakivalia barakoa na kudumisha umbali wa zaidi ya mita moja na nusu kati yao.
Baada ya mipira kunyunyuziwa dawa na ‘maball-boy’ mwishoni mwa kipindi cha kwanza, kipindi cha pili kilirejelewa kimyakimya huku kipenga cha refa kikisalia kuwa cha pekee kilichosikika.
Kuahirishwa kwa kampeni za Bundesliga kulifanyika wakati ambapo Bayern ambao kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 58, walikuwa wakijivunia fomu nzuri iliyowawezesha kusajili ushindi mara 10 kutokana na jumla ya mechi 11 mfululizo.
Kabla ya kuvaana na Union Berlin, mchuano wao wa mwisho kutandaza katika Bundesliga ulikuwa dhidi ya Augsburg waliopokea kichapo cha 2-0 ugani Allianz Arena mnamo Machi 8. Awali, walikuwa wamewatandika Chelsea 3-0 katika mkondo wa kwanza wa mwondoano wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na kuwabandua Schalke kwenye robo-fainali za German Cup.
Chini ya kocha mpya Hansi Flick, Bayern sasa wamefaulu kujizolea jumla ya alama 34 kutokana na jumla ya 36 walizokuwa na uwezo wa kutia kapuni kutokana na mechi 12 zilizopita.
Mgongo wao unasomwa kwa karibu sana na Borussia Dortmund na Borussia Monchengladbach wanaojivunia alama 54 na 52 mtawalia.
Tangu Disemba 7, 2019, walipopepetwa 2-1 na Borussia Monchengladbach, hakuna kikosi kingine chochote ambacho kimewazidia Bayern maarifa katika mapambano yote ya muhula huu.
Zikisalia mechi nane pekee kwa msimu huu wa Bundesliga kutamatika rasmi, Union Berlin wanashikilia nafasi ya 12 jedwalini kwa alama 30 huku pengo la pointi 17 likitamalaki kati yao na Bayer Leverkusen watakaokuwa wageni wa Werder Bremen mnamo Mei 18, 2020.
Likizo ya miezi miwili iliyopita imempa mvamizi Robert Lewandowski wa Bayern nafasi ya kupona jeraha la goti. Nyota huyo mzawa wa Poland ndiye mfungaji bora wa Bundesliga hadi kufikia sasa msimu huu kwa mabao 26.
Bayern walikosa huduma za kiungo Philippe Coutinho aliyefanyiwa upasuaji wa kifundo cha mguu majuzi. Nafasi yake ilitwaliwa na Kingsley Coman aliyeshirikiana vilivyo na Thiago Alcantara, Serge Gnabry na Thomas Muller katika safu ya kati.
MATOKEO YA BUNDESLIGA
Cologne 2-2 Mainz
Union Berlin 0-2 Bayern
Dortmund 4-0 Schalke
Augsburg 1-2 Wolfsburg
Dusseldorf 0-0 Paderborn
Leipzig 1-1 Freiburg
Hoffenheim 0-3 Hertha Berlin
Frankfurt 1-3 M’gladbach