Miaka yote nimeishi kutamani kuchezea Arsenal; nina raha sana, asema sajili mpya Calafiori
BEKI matata wa kimataifa, Riccardo Calafiori wa Italia amesema imekuwa ndoto yake kuchezea klabu ya Arsenal tangu akiwa na umri wa miaka 12.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 22 amejiunga na Arsenal kwa mkataba wa muda mrefu akitokea klabu ya Bologna ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kwa kandarasi iliyogharimu kiasi cha Sh4.2 bilioni pamoja na nyongeza nyingine za marupurupu.
Akichezea Arsenal, Calafiori aliyekuwa katika kikosi cha Italia kilichoshiriki Euro 2024, atakuwa akivalia jezi nambari 33 kuanzia msimu ujao wa 2024/2025.
“Beki wa kimataifa Riccardo Calafiori amejiunga nasi kutoka Bologna ya Serie A kwa mkataba wa muda mrefu,” taarifa fupi ya klabu ya Arsenal ilisema.
Calafiori alikuwa nguzo ya safu ya Bologna, akiibuka kama mmoja wa wachezaji wenye nguvu na thabiti katika ligi ya Serie A, lakini kocha Mikel Arteta amesisitiza kwamba hatamharakisha kucheza Jumatano dhidi ya Liverpool ugani Lincoln Financial Field.
“Huu ni mwanzo wa mambo makubwa zaidi maishani mwangu, kwa hakika nimefurahia kujiunga na Arsenal, timu niliyopenda tangu nikiwa mtoto mdogo,” alisema staa huyo aliyetambulishwa kwa wachezaji wenzake ugani Philadelphia Union Subaru Park ambapo kikosi cha Arsenal kimepiga kambi ya mazoezi kujinoa kwa msimu mpya.
“Nilizungumza na kocha pamoja na Edu (mkurugenzi wa michezo wa klabu) ambapo niliwaeleza hamu yangu ya kutaka kujiunga na Arsenal haraka iwezekanavyo,” alisema beki huyo.
“Kuna klabu nyingi zilizonihitaji, lakini sasa nimetua mahali nilikotaka. Niko hapa kwa ajili ya kusaidia Arsenal kutwaa mataji. Naipenda hii timu kwa sababu ina wachezaji wengi wa umri mdogo ambao watanipa matumaini makubwa ya kushinda mataji,” aliongeza Calafiori.
“Naweza kucheza katika nafasi tofauti. Popote kocha ataniweka, nitacheza. Nilishuhudia Arsenal ikicheza na Crystal Palace nikafurahia uchezaji wao. Nitajitahidi mazoezini ili nirejee katika kiwango changu bora, huku nikitarajia kusaidia timu kikamilifu,” alisema.
Usajili wake umekuja wakati kiungo Emile Smith Rowe anaondoka kujiunga na Fulham kwa mkataba unaosemekana kuwa wa thamani ya Sh3.4 bilioni pamoja na nyongeza za marupurupu.
Juhudi za Arsenal kumshawishi Rowe asalie klabuni ziligonga mwamba baada ya nyota huyo kukataa akisisitiza lazima atafute maisha mapya kwingineko.
Akizungumza kuhusu shughuli za usajili, kocha Arteta alisema hana mpango wa kuleta mastaa kwa sasa.
“Iwapo itawezekana, tutaimarisha kikosi, lakini kwa sasa nimetosheka na wachezaji nilionao. Hatutarajii kuleta majina makubwa kiwango cha akina Declan Rice kwa sasa.”
“Tuligundua ulegevu wetu kikosini mwezi Februari na Machi,” alisema Arteta, ingawa kulikuwa na uvumi kwamba Mhispania huyo anamfuatilia mshambuliaji Victor Osimhen wa Napoli mwenye umri wa miaka 25.
Wakati huo huo, mshambuliaji Julian Alvarez amesema ataamua hali yake ya baadaye baada ya kumalizika kwa Michezo ya Olimpiki za Paris 2024.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 alitarajiwa kuwa kikosini dhidi ya Ukraine jana katika mechi ya Olimpiki jijini Lyon.