Michezo

Mihic akiri presha inamlea, Gor ikiendea Mara Sugar KPL leo

Na CECIL ODONGO April 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KOCHA wa Gor Mahia Sinisa Mihic Jumamosi  alikiri kuwa presha inaendelea kumlemea katika juhudi za  klabu ya kutetea taji lake la  Ligi Kuu (KPL).

Mihic, 48 amekiri kuwa wakiendelea kudondosha alama, basi watajipata pabaya na kupoteza taji hilo ambalo Gor imelichukua mara 22.

Mihic atarejea kwenye benchi ya kiufundi ya Gor Jumapili baada ya kukosa sare ya 1-1 dhidi ya Sofapaka na kupigwa 1-0 na limbukeni FC Talanta mnamo Alhamisi uga huo huo wa Dandora.

Kocha huyo alipewa kadi nyekundi kwenye ushindi wa 1-0 dhidi ya KCB ndiposa hakuwa kwenye benchi katika michuano hiyo miwili.

“Presha imezidi na sasa lazima tushinde mechi zetu kwa sababu kila kitu kinatuwia vigumu. Najua mashabiki wamevunjika moyo na sasa ni wajibu wa kila mtu kujituma uli tuyapate matokeo mazuri,” akasema Mihic.

Kocha huyo alijizuia kuzungumzia uhasama ambao upo kwenye benchi ya kiufundi  huku baadhi ya mashabiki wakimtaka naibu wake Zedekiah ‘Zico’ Otieno aondoke klabuni humo.

K’Ogalo iliipiga Mara Sugar 2-0 kwenye mechi ya mkondo wa kwanza Novemba 30 mwaka uliopita. Mashabiki wametoa onyo kuwa Gor isiposhinda Mara Sugar mnamo Jumapili, basi benchi ya kiufundi na wachezaji wajiandae kukimbia.

Kenya Police inaongoza KPL kwa alama 52, huku Tusker ikivaana na Mathare United Jumapili ikilenga pia kurejea kileleni   Gor wakiwa na alama 47 wapo nambari tatu.

RATIBA YA JUMAPILI

JUMAPILI

Kakamega Homeboyz v Sofapaka (Mumias Sports Complex, Kakamega 2pm)

Ulinzi Stars v FC Talanta (Ulinzi Sports Complex, Nairobi 3pm)

Mathare United v Tusker (Dandora, Nairobi, 1pm)

Gor Mahia v Mara Sugar (Dandora, 4pm)